DAKTARI WA JIJI LA ARUSHA ATUHUMIWA KUMBAKA MTOTO WAKE, MAMA AELEZA MKASA MZIMA KWA UCHUNGU
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MAMA mmoja , Mchungaji Nembrisi Lukumay Mkazi wa jijini Arusha ameiomba serikali na vyombo vya sheria kuhakikisha haki inatendeka baada ya baba mzazi wa mtoto wake mwenye umri miaka 12 mwanafunzi wa darasa la saba,kutuhumiwa kumbaka mtoto huyo nyumbani huku familia ikiwa imeenda ibadani.
Akisimulia tukio hilo kwa uchungu, mtoto huyo mwanafunzi wa darasa la saba alisema tukio hilo lilitokea Aprili 9, 2026 baada ya ndugu wengine kwenda kanisani na kubaki nyumbani akiwa na baba yake.
Mtoto huyo alidai baba yake alimuita sebuleni, akamfungia mlango, akazima televisheni kisha kumfanyia kitendo hicho kabla ya kumpa Sh500 kwa ajili ya kununua biskuti na kumtaka asimweleze mtu yeyote, hata mama yake.
“Aliniambia nisimuambie mtu yeyote, hata mama, vinginevyo atanipiga,” alidai mtoto huyo.
Kwa mujibu wa mtoto huyo, baada ya tukio hilo alianza kuwa na hofu na kujitenga huku akionyesha mabadiliko ya kitabia yaliyomfanya mama yake kuanza kupata wasiwasi.
Mama wa mtoto huyo,Nabii Nembrisi Lukumay mkazi wa Ngusero jijini Arusha,alisema alianza kugundua hali isiyo ya kawaida kwa mwanawe kutokana na kuwa mwenye huzuni, kukosa amani na kuonekana mwenye maumivu.
Alisema baada ya kumbana mtoto huyo kwa maswali kwa siku kadhaa ndipo alipofanikiwa kueleza kuwa alikuwa amefanyiwa ukatili huo na baba yake mzazi.
“Niligundua mtoto hana amani kabisa. Nilipomchunguza niliona hali siyo ya kawaida ndipo nikaanza kumhoji kwa kina mpaka akaniambia ukweli,” alisema mama huyo kwa masikitiko.
Mama huyo ambaye alimtaja mumewe kwa jina la Antony Charles Mao ambaye ni daktari mfawidhi wa hospitali moja za jiji la Arusha,alisema baada ya kupata taarifa hizo alimhoji mume ambaye alikataa kata kata kuhusika na tukio hilo akimweleza kuwa hawezi kufanya kitendo hicho kwa binti ambaye ni mtoto wake.
Hata hivyo mama huyo ambaye ana watoto watatu na mtuhumiwa,alienda Kituo Kikuu cha Polisi Arusha (Central Police) ambapo alipokelewa na kupewa hati ya matibabu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika Hospitali ya Mount Meru.
Alisema vipimo vya kitabibu vilithibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa amefanyiwa ukatili wa kingono.
Aidha, mama huyo alidai kuwa licha ya kuripoti tukio hilo, ana hofu kuwa haki inaweza isipatikane kwa sababu mtuhumiwa huyo ni daktari anayefanya kazi jijini Arusha.
Mtoto huyo pia aliomba serikali iingilie kati kwa madai kuwa anaishi kwa hofu na wasiwasi juu ya usalama wake.
“Naomba serikali inisaidie kwa sababu bado ninaogopa baba yangu anaweza kunifanyia kitu kibaya,” alisema mtoto huyo.
Mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana na anadaiwa kujificha nyumbani kwa rafiki yake .
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku hatua za kisheria zikisubiriwa dhidi ya mtuhumiwa huyo kupitia taarifa ya polisi iliyofunguliwa kituo kikuu cha polisi jijini Arusha.AR|RB|4077|2026
Ends..


0 Comments