NGOBEI ATOA ONYO KWA WANAOKWAMISHA UCHANGIAJI WA MIRADI YA MAJI LONGIDO
Na Joseph Ngilisho, LONGIDO
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Thomas Ngobei, ametoa onyo kali kwa viongozi na wananchi wanaokwamisha uchangiaji wa fedha za miradi ya maji, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya yeyote anayehujumu juhudi za kuboresha huduma ya maji katika wilaya hiyo.
Ngobei alitoa kauli hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido wakati taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) ilipowasilishwa mbele ya baraza hilo.
Alisema ni lazima kamati za maji ziundwe kuanzia ngazi ya vijiji hadi kata ili kusimamia kikamilifu shughuli za maji pamoja na ukusanyaji wa michango ya wananchi kwa ajili ya kuendeleza huduma hiyo muhimu.
“Kamati hizi lazima ziundwe na zisimamiwe kikamilifu hadi ngazi ya vijiji na kata. Hatuwezi kufanikiwa katika sekta ya maji kama hakutakuwa na usimamizi madhubuti na ushirikishwaji wa wananchi,” alisema Ngobei.
Aidha, alisema hakuna kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kuzuia wananchi kuchangia fedha za maji kwa kuwa tayari sheria na sera za maji zimeweka utaratibu unaotambua vyombo hivyo kama wasimamizi halali wa huduma za maji.
“Hakuna mtu anayepaswa kuzuia uchangiaji wa maji. Sheria ipo wazi na hatua za kisheria zichukuliwe kwa yeyote anayekwamisha michango au usimamizi wa miradi ya maji,” alisisitiza.
Ngobei alisema baadhi ya maeneo bado yana changamoto ya wananchi kushindwa kuchangia huduma za maji, hususan kipindi cha mvua ambapo wafugaji wengi hutegemea maji ya mabwawa na silanja badala ya kutumia huduma za maji zinazolipiwa.
Alieleza kuwa hali hiyo husababisha kushuka kwa mapato ya miradi ya maji katika baadhi ya miezi, jambo linaloweza kuathiri uendeshaji wa huduma hiyo iwapo elimu kwa wananchi haitatolewa ipasavyo.
“Tunafahamu kipindi cha masika baadhi ya wananchi hasa wafugaji hutumia maji ya mabwawa na silanja, hivyo mapato hupungua. Lakini jambo la msingi ni kuendelea kutoa elimu na kuhakikisha wananchi wanatambua kuwa maji ni uhai,” alisema.
Pia aliwataka madiwani, viongozi wa vijiji na kata kushirikiana kwa karibu na AUWSA katika kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kuimarika na wananchi wanapata maji safi na salama kwa uhakika.




إرسال تعليق