NGOBEI ATAKA SERIKALI KUELEKEZA NGUVU KATIKA WILAYA YA LONGIDO ILI KUBORESHA BARABARA KUUNGANISHA KATA AMBAZO HAZIFIKIKI

 BARAZA LA MADIWANI LONGIDO LAIOMBA SERIKALI KUONGEZA FEDHA TARURA KUREKEBISHA BARABARA ZILIZOHARIBIWA NA MVUA

Na Joseph Ngilisho – LONGIDO

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido limeiomba serikali kuelekeza nguvu zaidi katika wilaya hiyo kwa kuongeza fedha za kutosha kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kurekebisha mtandao wa barabara ulioharibiwa vibaya na mvua za masika, hali iliyosababisha baadhi ya kata kutofikika kirahisi.

Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Thomas Ngobei, wakati wa kufunga kikao cha Baraza la Madiwani ambapo alisema changamoto ya miundombinu imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi kupata huduma muhimu pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ngobei alisema baadhi ya maeneo yamekatika kabisa kutokana na ubovu mkubwa wa barabara huku kata za ELang’atadapash  na ILorienito zikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi.





“Tunaiomba serikali kuitazama Longido kwa upekee katika kipindi hiki cha dharura. Kuna kata ambazo kwa sasa hazifikiwi kabisa kutokana na hali mbaya ya barabara baada ya mvua kubwa zilizonyesha,” alisema Ngobei.

Aidha, alisema uharibifu huo wa miundombinu unaathiri shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayohitaji usafiri wa uhakika.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo aliwataka viongozi wa taasisi mbalimbali wilayani humo kushiriki kikamilifu katika vikao vya kamati za halmashauri ili kuongeza ushirikiano katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alitolea mfano mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Engikareti akisema mafanikio yake yanategemea uwepo wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji na umeme.

“Huwezi kujenga sekondari kama hakuna barabara, maji wala umeme. Ushirikiano wa taasisi mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha miradi yetu inatekelezwa kwa mafanikio,” alisema.

Pia aliwapongeza wataalamu wa halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji kwa maandalizi mazuri ya taarifa za kikao na usimamizi wa mijadala iliyowezesha kikao kwenda kwa utulivu na ufanisi mkubwa.

Post a Comment

0 Comments