DC KALLI AHIMIZA USIMAMIZI WA MAPATO NA MIRADI YA MAENDELEO LONGIDO

 DC KALLI AHIMIZA USIMAMIZI WA MAPATO NA MIRADI YA MAENDELEO LONGIDO

Na Joseph Ngilisho, LONGIDO

MKUU wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli, amewataka madiwani, watendaji na viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kunufaika na fedha zinazotolewa na Serikali.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Kalli alisema kikao hicho kimekuwa na utulivu mkubwa huku wajumbe wakitoa hoja za kujenga zinazolenga kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo.



Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Longido imejipanga kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 5.2 katika mwaka wa fedha 2024/2025 na kwamba viongozi wote wanapaswa kuongeza juhudi ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa kabla ya kuanza mwaka mpya wa fedha.

“Kuna muda mfupi uliobaki, hivyo ni lazima tukaze usimamizi wa mapato yetu na kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinakwenda kutekeleza miradi iliyokusudiwa,” alisema Kalli.

Alieleza kuwa asilimia 20 ya mapato ya ndani ya halmashauri yanaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo katika kata, vijiji na vitongoji, huku akisisitiza kuwa madiwani wanapaswa kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha hizo.

“Madiwani tembeleeni vijiji vyenu, kaeni na kamati za maendeleo na fuatilieni miradi inayotekelezwa ili wananchi waone thamani ya fedha zao,” alisema.

Kalli pia alisisitiza umuhimu wa uwazi katika matumizi ya fedha za maendeleo kwa kuwataka viongozi wa vijiji kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia kutopatiwa taarifa za fedha zinazotolewa kwenye maeneo yao, jambo ambalo linaweza kuondoa imani kwa viongozi iwapo halitapatiwa ufumbuzi.

Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Wilaya aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo wilayani humo ikiwemo miradi ya umeme, afya, elimu na miundombinu ya barabara.

Alisema vijiji vyote vya Wilaya ya Longido tayari vimefikiwa na huduma ya umeme huku juhudi zikielekezwa sasa kwenye vitongoji ambavyo bado havijapata huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Kalli, kati ya vitongoji 174 vya wilaya hiyo, zaidi ya vitongoji 113 tayari vina umeme na wakandarasi wanatarajiwa kuanza kazi katika vitongoji vilivyobaki kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

Aidha, alieleza kuwa Serikali tayari imetoa zaidi ya shilingi milioni 529 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kisasa katika eneo la Engikareti, mradi ambao unatarajiwa kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wa wilaya hiyo.


Aliwataka viongozi wote kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilika kwa wakati na kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Longido.


Ends..

Post a Comment

0 Comments