MWEKEZAJI WA MANYARA SAFARI LODGE ALALAMIKIA TISHIO LA USALAMA, MPANGAJI AGOMA KUHAMA NYUMBA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWEKEZAJI wa kigeni na mmiliki mwenza wa jengo la biashara la Manyara Safari Lodge- heritage camp lodge's lililopo wilayani Karatu, mkoani Arusha, Timothy Flavell amelalamikia kile alichodai ni jaribio la kutapeliwa na mpangaji wake, Erick Mashauri, anayeshikilia eneo hilo licha ya kuvunjwa kwa mkataba wa upangaji.
Flavell, raia wa Uingereza aliyeoa na kuishi Tanzania, alisema mpangaji huyo aliingia mkataba mwaka 2022 lakini ameshindwa kulipa kodi ya pango inayodaiwa kufikia zaidi ya dola za Marekani milioni 26, hali iliyowalazimu kusitisha rasmi mkataba huo kuanzia Aprili 1, 2026.
Kupitia kampuni yao ya Tarylin Ltd, inayomiliki pia Manyara Safari Lodge, Flavell alisema wametoa notisi kadhaa za maandishi, ikiwemo tangazo kwenye gazeti la serikali, lakini mpangaji huyo ameendelea kukaidi kuondoka na badala yake kudai kuwa yeye ni mwekezaji.
“Tumefuata taratibu zote za kisheria, lakini bado anakataa kuondoka na hata anatishia usalama wetu. Tunaiomba serikali iingilie kati,” alisema Flavell.
Aliongeza kuwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, mpangaji huyo alijieleza kuwa si mpangaji bali ni mwekezaji aliyejenga baadhi ya miundombinu ya lodge hiyo—madai ambayo Flavell aliyakanusha.
Kwa mujibu wa Flavell, mkataba wa awali ulimtaka mpangaji kulipa dola 25,000 kwa mwaka pamoja na asilimia 10 ya mapato kwa kila mgeni, lakini mwaka jana alianza kuchelewesha malipo na baadaye kulipa asilimia 5 bila makubaliano.
Aidha, alidai mpangaji huyo alijenga vyumba viwili na kudai gharama ya dola 70,000, lakini mmiliki anasisitiza kuwa thamani ya ujenzi huo ni ndogo kuliko inavyodaiwa.
Flavell alisema baada ya kusitishwa kwa mkataba, walifanikiwa kumwondoa mpangaji huyo kwa msaada wa walinzi binafsi, lakini baadaye alirejeshwa kufuatia maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ili kumalizia wateja waliokuwa tayari wameweka nafasi.
Akizungumzia mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, alikiri kuufahamu na kusema alitoa maelekezo ya mpito kwa lengo la kulinda amani na maslahi ya wageni.
Alisema alimruhusu mpangaji kurejea kwa muda wa wiki mbili ili kukamilisha huduma kwa wageni waliokuwa tayari wamefanya booking, na baada ya hapo pande zote zielekezwe kutafuta haki kupitia vyombo vya sheria.
Akizungumza kwa uchungu na masikitiko, Flavell alisema amewekeza fedha nyingi katika uwekezaji huo kupitia usajili wake na Tanzania Investment Centre (TIC), akibainisha kuwa mali hiyo ndiyo tegemeo lake kuu kimaisha.
“Nimewekeza kila kitu nilichonacho katika mali hii. Nimekuja Tanzania kwa nia njema ya kuwekeza na kuchangia uchumi, lakini ninachokutana nacho sasa ni kudhulumiwa na si haki kabisa,” alisema.
Alidai kuwa mpangaji wake, Mashauri, ameshindwa kulipa kodi ya pango lakini bado anaendelea kushikilia jengo hilo, hali ambayo amesema inakiuka misingi ya haki na sheria, hususan baada ya yeye kuchukua hatua ya kurejea kwa amani (peaceful re-entry) kama inavyoruhusiwa kisheria.
Kwa mujibu wa Flavell, mbali na hasara ya kifedha, mgogoro huo umeathiri pia hali yake ya kiafya na kisaikolojia kutokana na vitisho anavyodai kupokea mara kwa mara.
“Sina tena amani. Siwezi kulala, kila nikisikia sauti usiku nahofia kuwa labda ni watu wanakuja kunichukua tena. Nimekuwa nikiishi kwa hofu kubwa,” alieleza.
Aidha, alisema amepewa shinikizo la kukabidhi funguo za jengo hilo, akitahadharishwa kuwa akishindwa kufanya hivyo, anaweza kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Nimeambiwa nikabidhi funguo, vinginevyo nitakamatwa na kuwekwa mahabusu. Niko tayari kufanya hivyo kwa sababu tayari nimeshawahi kupitia mchakato wa mahakama juu ya mali hii. Lakini ukweli ni kwamba, hili si jambo la haki,” alisisitiza.
Flavell amesema ametumia zaidi ya miaka kumi kujenga na kuendeleza uwekezaji huo, na hivyo kuiomba Serikali iingilie kati ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.
“Ninachoomba ni haki, ulinzi na usawa mbele ya sheria. Tafadhali nisaidieni,” alihitimisha.
Karanga aliwataka wawekezaji na wahusika wa mgogoro huo kujiepusha na migogoro inayoonekana hadharani, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inajiandaa kupokea wageni wengi kutokana na mashindano ya AFCON.
“Tusioneshe tofauti zetu mbele ya wageni. Tulinde taswira ya nchi yetu kwa kuonesha uzalendo na kuhakikisha wageni hawapati usumbufu wowote,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa hatua hiyo haimaanishi kumpa ushindi upande wowote bali ni jitihada za kuhakikisha amani inatawala huku taratibu za kisheria zikifuatwa.
Katika tukio la hivi karibuni, Flavell alidai kuwa mpangaji huyo alivamia eneo hilo akiwa na kundi la watu, akabomoa uzio na kuingia kwa nguvu huku akijaribu kumtoa ndani ya jengo hilo.
Hata hivyo, juhudi za kumpata Erick Mashauri kuzungumzia tuhuma hizo hazikufanikiwa hadi wakati wa kuchapisha habari hii.
Mgogoro huo unaendelea kufuatiliwa huku ukiibua mjadala kuhusu ulinzi wa mikataba ya biashara na mazingira ya uwekezaji nchini.
ENDS



إرسال تعليق