MWAMNYANGE AIMWAGIA SIFA LUKUKI HALMASHAURI LONGIDO,ASEMA HAKUWAHI KUONA BARAZA LA MADIWANI LENYE UTULIVU KAMA HILO,AOMBA USHIRIKIANO

 KATIBU TAWALA MSAIDIZI ARUSHA AIPONGEZA HALMASHAURI YA LONGIDO KWA UENDESHAJI WA BARAZA

Na Joseph Ngilisho | LONGIDO

KATIBU Tawala Msaidizi anayeshughulikia Serikali za Mitaa Mkoa wa Arusha, Nsajigwa Wamunyange, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa namna inavyoendesha Baraza la Madiwani kwa utulivu, mshikamano na mijadala yenye kulenga maslahi ya wananchi.

Wamunyange alitoa pongezi hizo alipohudhuria kwa mara ya kwanza kikao cha baraza hilo la Madiwani tangu ahamishiwe Mkoa wa Arusha mwezi mmoja uliopita, akisema ameridhishwa na kiwango cha ushirikiano pamoja na namna madiwani wanavyotekeleza wajibu wao wa kuisimamia serikali na kuwatetea wananchi katika maeneo yao.

Alisema uzoefu alioukuta Longido umeonyesha mfano mzuri wa uendeshaji wa mabaraza ya madiwani tofauti na baadhi ya maeneo aliyowahi kufanya kazi, ambako vikao vilikumbwa na migogoro na kushindwa kuendelea kutokana na kutokuelewana.

“Naomba mnipokee na kunipa ushirikiano ule ule ambao mlimpa mtangulizi wangu hadi akatambulika na kupandishwa cheo. Nami nina matumaini ya kufanya kazi kwa karibu na baraza hili,” alisema Wamunyange.

Kabla ya kuhamishiwa Arusha, Wamunyange alikuwa akihudumu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha, huku nafasi hiyo aliyopo sasa ikishikiliwa awali na Ramadhani Madereka ambaye amehamishiwa Wizara ya TAMISEMI.

Aidha, aliwapongeza mwenyekiti wa halmashauri pamoja na madiwani kwa namna wanavyoendesha mijadala yenye tija na kuhimiza uwajibikaji wa viongozi, akieleza kuwa serikali iliunda mabaraza ya madiwani kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua changamoto katika ngazi za chini bila kusubiri maamuzi kutoka serikali kuu.

Kwa mujibu wa Wamunyange, awali alipowasili Mkoa wa Arusha alipata hofu kutokana na taarifa za changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika baadhi ya halmashauri, lakini baada ya kutembelea maeneo mbalimbali amebaini kuwa zipo halmashauri zinazofanya vizuri katika kusimamia maendeleo na kudumisha mshikamano wa kisiasa.

“Nimefanya kazi Lindi ,Mkoa wa Pwani na sasa Arusha. Nilipofika hapa nilikutana na changamoto katika baadhi ya maeneo na nikahisi mkoa huu ni mgumu, lakini kadri nilivyoendelea kutembelea halmashauri mbalimbali nimegundua kuna maeneo yanafanya vizuri sana,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka madiwani kuendelea kutumia maarifa waliyopewa kupitia mafunzo ya uendeshaji wa mabaraza kwa busara na weledi, akisisitiza kuwa tofauti za kimtazamo ndani ya vikao zinapaswa kuwa sehemu ya kuimarisha demokrasia na si chanzo cha migogoro isiyo na manufaa kwa wananchi.

Alisema mabaraza ya sasa yameendelea kupata mafunzo ya kina zaidi kuhusu sheria, taratibu na mbinu za uongozi, jambo ambalo linapaswa kusaidia kuongeza ubora wa mijadala na maamuzi yanayolenga maendeleo ya wananchi.

“Ni kawaida kwa mabaraza haya kukutana na tofauti za kimtazamo, lakini kikubwa ni kuhakikisha mijadala inabaki kuwa ya kujenga maendeleo ya wananchi na kuimarisha utoaji wa huduma,” alisisitiza.

Ends..

Post a Comment

أحدث أقدم