MTO WA MBU YAZAMA KWENYE MAFURIKO YA ZIWA MANYARA , KAYA 408, MAKANISA NA MAKABURI YAFUNIKWA KWENYE MAJI ,MBUNGE AWAFARIJI KWA MILIONI 3,KUBISHA HODI KWA WAZIRI MKUU

 KAYA 408, MAKANISA NA MAKABURI YAZINGIRWA NA MAFURIKO MTO WA MBU

Wananchi wakosa makazi, Mbunge Monduli akimbilia Ofisi ya Waziri Mkuu, awafariji kwa Sh milioni 3

Na Joseph Ngilisho|NONDULI

ZAIDI ya kaya 408 katika Kijiji cha Jangwani, Kata ya Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani Arusha zimezingirwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na kuongezeka kwa maji ya Ziwa Manyara, hali iliyosababisha mamia ya wananchi kukosa makazi huku makanisa, makaburi na mashamba yakivamiwa na maji.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa eneo hilo sasa wanaishi katika mazingira magumu wakihofia usalama wao, huku baadhi wakikosa sehemu salama za kuishi baada ya maji kuingia kwenye nyumba zao na kuharibu mali pamoja na mazao ya chakula.


Mbunge wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph Copriano, ameibuka kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kufika eneo hilo kujionea athari za mafuriko hayo, ambapo ametoa msaada wa Shilingi milioni tatu kwa ajili ya chakula cha waathirika huku akiahidi kuifikisha kero hiyo moja kwa moja Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Maafa.

Akizungumza jana baada ya kutembelea eneo lililoathirika, Copriano alisema serikali haiwezi kuwaacha wananchi wake katika mateso hayo na kuahidi kuwasilisha haraka taarifa ya maafa hayo kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba, ili hatua za dharura ziweze kuchukuliwa.

“Nawapeni pole sana kwa changamoto hii iliyowakuta. Ninaahidi kuwa kesho asubuhi nitagonga hodi Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Maafa ili wananchi hawa wapate msaada wa haraka. Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inaendelea kusikiliza wananchi wake,” alisema Copriano.


Mbunge huyo alisema mafuriko hayo si tu yameharibu nyumba za wananchi bali pia yameathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, baada ya maji kuzunguka maeneo ya ibada, makaburi na mashamba yaliyokuwa tegemeo kuu la chakula kwa wakazi wa kijiji hicho.

Wananchi waliozungumza kwa nyakati tofauti walieleza kuwa wamekuwa wakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Manyara, jambo linalowalazimu kuhama mara kwa mara na kupoteza mali zao kila msimu wa mvua unapokuwa mkubwa.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba serikali kuwapatia maeneo mapya ya makazi na kilimo yatakayokuwa salama dhidi ya mafuriko, wakipendekeza maeneo ya karibu na kambi za jeshi ambayo yamekuwa hayaguswi na maji hata wakati wa mvua kubwa.

Mbali na changamoto ya makazi, wananchi hao pia wameeleza hofu yao juu ya nguzo za umeme zilizozingirwa na maji, wakihofia kutokea kwa hitilafu za umeme au madhara ya shoti kwa wananchi na watoto wanaocheza karibu na maeneo hayo.

Kwa upande wake, Copriano alisema tayari amepokea ombi hilo na kuahidi kuwasiliana na Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO, pamoja na mamlaka nyingine husika ili kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa kuondoa hatari inayoweza kujitokeza.

Mafuriko hayo yanaendelea kuongeza hofu kwa wakazi wa Mto wa Mbu huku wananchi wakiiomba serikali kuharakisha msaada wa kibinadamu pamoja na mpango wa kudumu wa kuwaondoa katika maeneo hatarishi ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza kujitokeza siku zijazo.










Ends

Post a Comment

أحدث أقدم