MBUNGE LUKUMAY AIBANA SERIKALI KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI WA AFYA ARUMERU MAGHARIBI

 MBUNGE LUKUMAY AIBANA SERIKALI KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI WA AFYA ARUMERU MAGHARIBI

Na Joseph Ngilisho | Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lembulung Lukumay ameiiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya katika baadhi ya vituo vya afya vya jimbo hilo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akiuliza swali bungeni leo, Dkt. Lukumay alianza kwa kumshukuru Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tano ambazo zimewezesha ujenzi wa vituo vitano vya afya katika jimbo la Arumeru Magharibi.

Alisema kupitia fedha hizo, vituo vinne vya afya tayari vinaendelea kutoa huduma mbalimbali ikiwemo upasuaji kwa mama wajawazito, hatua ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.

Hata hivyo, mbunge huyo alieleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi wa afya katika baadhi ya vituo hivyo, hali inayowalazimu watumishi kuishi mbali na maeneo ya kazi.

“Vituo vitatu vya afya bado havina nyumba za watumishi, jambo linalosababisha wahudumu kuishi mbali na vituo hivyo na wakati mwingine kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Dkt. Lukumay.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni vya kata za Oldonyosambu, Mbuyuni, Olorien na Nduruma, ambapo wananchi wamekuwa wakihitaji huduma za afya kwa wakati hasa huduma za dharura na uzazi.

Kutokana na hali hiyo, alihoji ni lini Serikali itajenga nyumba za watumishi katika vituo hivyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Akijibu swali hilo, Naibu waziri wa Afya alisema Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha miundombinu ya afya nchini ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini.

Ends

Post a Comment

0 Comments