CRDB YAKABIDHI TISHEti 500, MIPIRA KWA POLISI JAMII JOGGING CLUB ARUSHA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
BENKI ya CRDB Bank Plc imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono shughuli za kijamii, afya na maendeleo kwa kukabidhi msaada wa tisheti 500 pamoja na mipira minne ya michezo kwa Polisi Jamii Jogging Club ya Arusha.
Msaada huo ulikabidhiwa na Meneja wa Kanda wa benki hiyo, Cosmas Sadat, kwa mlezi wa klabu hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Georgina Matagi, katika hafla iliyofanyika viwanja vya Polisi Wilaya ya Arusha na kuhudhuriwa na askari polisi pamoja na wananchi mbalimbali.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo katika viwanja vya polisi wilaya Arusha ,Sadat alisema CRDB inaamini michezo na mazoezi ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya, mshikamano wa jamii na mahusiano mema kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Alisema benki hiyo imekuwa mshirika wa karibu wa Polisi Jamii Jogging Club kupitia utoaji wa elimu ya fedha, huduma za biashara na uwezeshaji wa vikundi mbalimbali ili wananchi waweze kuinuka kiuchumi.
“Michezo ni biashara. Kupitia Polisi Jamii Jogging Club tumekuwa tukitoa elimu ya fedha kwa mtu mmoja mmoja na vikundi mbalimbali ili waweze kutimiza ndoto zao za kiuchumi,” alisema Sadat.
Aliongeza kuwa CRDB haitaki wananchi waishie kufanya mazoezi pekee, bali wanufaike pia na maarifa ya kifedha, ujasiriamali na huduma za benki zitakazowawezesha kuboresha maisha yao.
Kutokana na hali hiyo, Sadat alitoa rai kwa wakazi wa Arusha kujiunga na Polisi Jamii Jogging Club ili waweze kunufaika kiafya na kiuchumi kupitia fursa zinazotokana na ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha, ACP Salvas Makweli, alisema Arusha Jogging Club imeendelea kuwa mfano wa mafanikio nchini kutokana na ukuaji wake mkubwa, ushiriki wa wananchi wengi pamoja na uwezo wake wa kuvutia wadhamini.
Alisema klabu hiyo sasa imepata umaarufu mkubwa ndani na nje ya Mkoa wa Arusha kupitia shughuli zake zinazorushwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Kwa sasa club iko live sana. Ukiangalia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii utaona namna Arusha Jogging Club ilivyopata nguvu kubwa,” alisema ACP Makweli.
Aidha, alimpongeza Georgina Matagi pamoja na viongozi wa klabu hiyo kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya huku akiishukuru CRDB kwa kuendelea kuidhamini klabu hiyo.
ACP Makweli alisema michezo imeendelea kuwa daraja muhimu la kuunganisha jamii, kuimarisha afya na kutoa fursa kwa vijana kukuza vipaji vyao, huku Polisi Jamii ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha michezo inachochea maendeleo na mshikamano wa wananchi.
Naye mlezi wa Polisi Jamii Jogging Club ambaye pia ni OCD wa Arusha, Georgina Matagi, alisema klabu hiyo imekuwa kiungo muhimu cha kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi kupitia michezo na mazoezi.
Matagi alisema klabu hiyo yenye wanachama zaidi ya 300 imekuwa ikifanya mazoezi kila Jumamosi asubuhi huku ikihamasisha afya bora, amani, mshikamano na mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu katika jamii huku ikilenga mahusiano bora ya polisi na Raia.
Aliishukuru CRDB kwa kuendelea kuwa mdhamini mkubwa wa klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia mafanikio makubwa ya Polisi Jogging Club Arusha.
“Msaada huu utasaidia kuongeza hamasa kwa wanachama wetu na kuendeleza shughuli mbalimbali za kijamii tunazozifanya kupitia klabu hii,” alisema Matagi.
Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo walieleza kufurahishwa na msaada huo wakisema utawapa motisha zaidi ya kushiriki mazoezi pamoja na shughuli za maendeleo zinazofanywa na klabu hiyo.
Polisi Jamii Jogging Club ya Arusha imeendelea kuvutia mamia ya wananchi kushiriki mazoezi ya pamoja kila wiki huku ikijijengea sifa ya kuwa moja ya klabu zinazochochea afya, umoja na maendeleo ya kijamii katika Mkoa wa Arusha.
Ends..















0 Comments