ARUSHA YATIKISIKA: MKUTANO MKUBWA WA UAMSHO KUANZA KESHO KATIKA CALVARY TEMPLE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
JIJI la Arusha limeingia katika ukurasa mpya wa historia ya kiroho kufuatia kuanza rasmi kwa mkutano mkubwa wa uamsho ulioandaliwa na Kanisa la Calvary Temple, tukio linalotarajiwa kuvuta maelfu ya waumini na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi.
Mkutano huo unafanyika katika kanisa hilo kuanzia kesho May 21 hadi 24,Mwaka huu na unatajwa kuwa tukio maalum lenye lengo la kuleta mabadiliko ya kiroho, kijamii na kisaikolojia, hasa kwa vijana na familia wanaokabiliwa na changamoto kubwa katika nyakati za sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo May 20,2026 jijini Arusha, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo la Calvary Temple, Philip David, alisema mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya Juma la Pentekoste na unalenga kuleta mwamko mpya wa kiroho kwa wakazi wa jiji na maeneo ya jirani.
Waandaaji wanasema mkutano huo unafanyika wakati ambapo changamoto za afya ya akili kwa vijana zinaongezeka kwa kasi, huku wengi wakikumbwa na msongo wa mawazo, utegemezi wa dawa za kulevya na kupoteza mwelekeo wa maisha.
Kwa mujibu wa viongozi wa kanisa, tukio hilo linatarajiwa kuwa mwanzo wa wimbi la mabadiliko litakaloanzia Arusha na kuenea katika miji mingine ya Tanzania.
“Tunaamini Arusha imefikiwa na majira ya kipekee ya kiroho. Huu ni wakati wa Mungu kuutembelea mji wetu,” alisema mchungaji huyo.
Mkutano huo utamshirikisha mhubiri wa kimataifa,kutoka nchini Sweden,Johannes Amritzer mwenye ushuhuda wa kweli na wa kipekee aliyewahi kupitia changamoto za uraibu wa dawa za kulevya kabla ya kupata mabadiliko makubwa ya maisha.
Mhubiri huyo aliwahi kuishi katika sober house – makazi maalum ya kusaidia waathirika wa uraibu kuacha matumizi ya dawa za kulevya – na sasa anahubiri injili na kuwahamasisha vijana kubadilisha maisha yao.
Waandaaji wanaamini ushuhuda wa maisha halisi una nguvu zaidi kuliko mafundisho ya nadharia katika kuwafikia vijana waliokata tamaa.
Mkutano huo utaongozwa na mwinjilisti wa kimataifa kutoka Sweden, Johannes Amritzer, anayejulikana kwa kuhubiri katika mikutano mikubwa inayohudhuriwa na maelfu hadi mamia ya maelfu ya watu duniani.
Mara baada ya kuwasili Arusha, alisema amefurahishwa na mapokezi mazuri aliyoyapata na kusisitiza kuwa washiriki wa mkutano huo watakuwa “wainjilisti” watakaobeba ujumbe wa injili katika ukanda mzima.
Katika ushuhuda wake, Amritzer alisimulia maisha yake ya utotoni yenye changamoto nyingi, akieleza kuwa aliishi maisha ya upweke na ulevi kwa miaka kadhaa kabla ya kubadilishwa na imani ya Kikristo baada ya kukutana na mke wake Maria aliyemwelekeza kanisani.
Alisisitiza kuwa mkutano huo ni wa watu wote bila kujali dini, akiwakaribisha hata marafiki wa Kiislamu na jamii nzima kuhudhuria kusikiliza ujumbe wa tumaini na upendo.
Huduma ya sifa na kuabudu itaongozwa na mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili Tanzania, Upendo Nkone, anayetarajiwa kutoa huduma maalum ya muziki.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema mkutano huo si wa kawaida bali ni wakati wa Mungu kufanya mambo makubwa ya uponyaji, wokovu na faraja kwa watu.
“Huu ni mkutano wa nguvu ya Roho Mtakatifu. Tunataka kugusa maisha ya wengi,” alisema.
Katika kauli iliyovuta hisia za waandishi, Upendo alitoa wito kwa wahudumu wa injili kuepuka kuigeuza huduma kuwa biashara, akisisitiza kuwa Mungu ndiye Hakimu wa haki.
Waandaaji wametenga siku ya Jumamosi kuwa maalum kwa vijana na wanafunzi wa shule na vyuo, wakitaja kuwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ni vijana chini ya miaka 30.
“Hatuwezi kuwaacha vijana nyuma. Tunataka wapokee Neno la Mungu na kupata mwelekeo mpya wa maisha,” alisema mchungaji huyo.
Maandalizi ya usafiri maalum yamefanyika kuhakikisha vijana wengi wanapata fursa ya kushiriki mkutano huo.
Viongozi wa kanisa wanasema mkutano huo hautalenga miujiza pekee bali kuhimiza uamsho wa kiroho kama msingi wa mabadiliko ya kudumu ya jamii.
Kwa mtazamo wao:Uamsho huleta mabadiliko ya maishaMabadiliko huleta matumaini ,Matumaini hujenga jamii imara,Wanasisitiza kuwa lengo kuu ni kumkazia “Mtenda miujiza” badala ya miujiza yenyewe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Emmanuel Elias, amesema maandalizi ya mkutano wa siku nne yamekamilika na watumishi wote waliokaribishwa tayari wamewasili.
Amehimiza wananchi na waumini kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo unaoanza rasmi kesho saa kumi na mbili jioni.
**Mwisho**













0 Comments