AJALI YA RC SHINYANGA YAUA MWANDISHI WA HABARI SABA WAJERUHIWA YUMO WA ITV

 MWANDISHI AFARIKI AJALI YA MSAFARA WA RC SHINYANGA, SABA WAJERUHIWA

Na Joseph Ngilisho | SHINYANGA

Msiba mkubwa umeikumba sekta ya habari mkoani Shinyanga baada ya mpiga picha wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Boaz Martine, kufariki dunia katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Mei 19, 2026 katika Kata ya Samuye, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Katika ajali hiyo, watu saba akiwemo mwandishi wa habari wa ITV/Radio One, Frank Mshana, walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba T.210 EDB pamoja na Toyota Land Cruiser Hardtop lenye namba DFPA 8920 mali ya Shirika la KOICA, lililokuwa limewabeba waandishi wa habari pamoja na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 20, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Harrier aliyekuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.

Alisema kutokana na uzembe huo, gari hilo liligongana na Land Cruiser Hardtop lililokuwa katika msafara huo, hali iliyosababisha kifo cha Boaz Martine na majeraha kwa watu wengine saba.

Majeruhi waliotajwa ni Frank Mshana, Johnson James, Koplo Swahiba Msangi, Neema Madono (36), Rehema Edson (45), Shadia Omari (32) pamoja na dereva wa Land Cruiser Hardtop, Laurence Peter (34).

Kwa mujibu wa RPC Magomi, majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga huku hali zao zikiendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limetoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa wanapofanya majaribio ya kuyapita magari mengine, ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo na majeruhi.

Ajali hiyo imeibua huzuni kubwa miongoni mwa waandishi wa habari na watumishi wa serikali mkoani humo kutokana na mchango wa marehemu Boaz Martine katika shughuli za habari na mawasiliano ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Ends

Post a Comment

0 Comments