AFRIKA STAR YAZINDUA RASMI “BABKUBWA LA WASUSI SEASON 2” ARUSHA, YAAHIDI KUWAWEZESHA WASUSI NCHI NZIMA

 AFRIKA STAR YAZINDUA RASMI “BABKUBWA LA WASUSI SEASON 2” ARUSHA, YAAHIDI KUWAWEZESHA WASUSI NCHI NZIMA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

KAMPUNI ya Afrika Star kupitia kampeni yake ya “Babkubwa la Wasusi Season 2” imeendelea kutoa mafunzo na fursa za kiuchumi kwa wasusi nchini baada ya kuzindua rasmi semina yake katika mikoa ya Kaskazini huku ikiwataka wasusi kutumia taaluma yao kama biashara yenye uwezo wa kuwainua kiuchumi.

Akizungumza jijini Arusha katika semina iliyowajutanisha wasusi zaidi ya 300, Meneja wa Mauzo na Masoko wa kampuni ya Afrika Star , HADI HAMADY alisema kuwa semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo wasusi pamoja na kuwafungulia njia mpya za biashara kupitia bidhaa na huduma zinazotolewa na kampuni hiyo.

Alisema msimu wa pili wa “Babkubwa la Wasusi” umeanza rasmi baada ya kampuni hiyo kufanya ziara katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Iringa, Dodoma, Kahama na Mwanza kabla ya kufika Arusha, huku hatua inayofuata ikiwa ni Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kufunga rasmi jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka huu.

“Kampeni hii ni maalum kwa ajili ya wasusi na wamiliki wa saluni nchini kote. Lengo letu ni kuwawezesha, kuwajengea kujiamini na kuwapa fursa za kukuza biashara zao. Haya ni maandalizi ambayo tutakuwa tukiyafanya kila mwaka mwezi wa tano kupitia semina mbalimbali nchi nzima,” alisema.

Alieleza kuwa mwitikio kutoka kwa wasusi umekuwa mkubwa katika kila mkoa wanaopita huku wengi wakionesha hamasa na matarajio makubwa ya kushiriki katika programu hiyo ambayo imekuwa ikitoa elimu pamoja na zawadi mbalimbali kwa washiriki.


“Tumepokelewa vizuri sana kila tunapofika. Wasusi wanafurahia na wanasubiri kwa hamu ujio wetu katika mikoa yao. Tunaamini mpaka tunamaliza ziara yetu tutakuwa tumewafikia zaidi ya wasusi 2,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania,” alisema.

Aidha alisema kuwa mbali na kutoa elimu ya ususi, kampuni hiyo inalenga kuwabadilisha wasusi kutoka kuwa watoa huduma wa kawaida na kuwa wafanyabiashara wenye uwezo wa kuuza bidhaa mbalimbali zinazohusiana na urembo.

Alisema Afrika Star ilianzisha kampuni ya usambazaji mwaka 2023 kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wasusi nchini ambapo kwa sasa wamefungua maduka na vituo vya usambazaji katika mikoa mbalimbali ili kupunguza gharama za usafirishaji na kuhakikisha bidhaa zinawafikia kwa wakati na kwa bei ya kiwandani.

“Sasa wasusi wana nafasi ya kununua bidhaa kwa bei ya jumla na kuziuza kwa bei ya rejareja. Hii inawasaidia kuongeza kipato na kukuza biashara zao,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema kupitia mpango wa “Babkubwa la Wasusi Season 2”, kampuni hiyo imeanzisha mfumo wa kukusanya pointi kupitia lebo za bidhaa zao ambapo wasusi wanaweza kubadilisha lebo hizo na kupata zawadi mbalimbali ikiwemo televisheni, simu janja pamoja na vifaa vingine vya matumizi.

Aliongeza kuwa tofauti na programu nyingine, wao wameongeza thamani zaidi kwa kutoa fedha taslimu papo hapo kwa washiriki wanaokusanya pointi kupitia lebo hizo.

“Lebo yako ni mtaji wako. Kila lebo ina thamani yake. Unapobadilisha lebo na pointi unapata zawadi au fedha taslimu hapo hapo,” alisema.

Afrika Star imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuwainua wasusi wa Tanzania kwa kuwapatia elimu, mitaji ya biashara na fursa za ukuaji wa kiuchumi kupitia sekta ya urembo ambayo inaendelea kukua kwa kasi nchini.



**Ends**

Post a Comment

أحدث أقدم