ZARA TOURS NA TATO WAKISHIRIKI KUINUA UBORA WA UTALII TANZANIA, WAIPONGEZA SERIKALI KWA MAENDELEO MAKUBWA SEKTA YA UTALII
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
KAMPUNI ya utalii ya Zara Tours, mojawapo ya kampuni zinazoongoza katika sekta ya utalii Tanzania, imeendelea kuonesha mchango wake mkubwa katika kukuza ubora wa huduma na kuimarisha taswira ya nchi katika soko la kimataifa la utalii, huku ikiiunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni hiyo, jijini Arusha,Mkurugenzi wa Zara Tours, Zainab Ansell ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za makusudi katika kuimarisha sekta ya utalii, akisema mafanikio yanayoendelea kuonekana yanatokana na ushirikiano thabiti kati ya Serikali na sekta binafsi.
Alisema Zara Tours inajivunia kuwa sehemu ya maendeleo ya sekta hiyo kupitia uwekezaji wake katika kuboresha huduma, kutoa mafunzo kwa watumishi, na kuhakikisha wageni wanaopata huduma zao wanabaki kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania duniani.
“Hii ni hatua kubwa sana kwa sekta yetu. Tunapoongelea utalii bora, tunamaanisha kuwaandaa wale wanaokutana moja kwa moja na wageni wetu. Mafunzo haya yanakwenda kuboresha kwa kiwango kikubwa ubora wa huduma na taswira ya nchi yetu,” alisema Zainabu.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kitaifa za kuinua ubora wa utalii, hususan kupitia mafunzo na ubunifu wa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa, akisisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu ni msingi muhimu wa mafanikio ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO), ambacho ndicho waandaaji wa mafunzo kwa waongoza watalii na madereva wa watalii, kimesema lengo la programu hiyo ni kuwajengea uwezo na kuwanoa vijana ili wawe tayari kukabiliana na msimu mpya wa utalii nchini, sambamba na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.
Akizungumza kwa niaba ya TATO, Mkurugenzi Mtendaji wake, Elirehema Maturo, alisema mafunzo hayo yaliyofunguliwa na waziri wa Maliasili na Utalii ,Ashatu Kijaji jijini hapa, yatanufaisha wadau wa utalii wapatao 2,000 nchini, wakiwemo waongoza watalii na madereva, hatua ambayo ni muhimu katika kuinua ubora wa huduma katika sekta hiyo nyeti.
Alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka, yakiwa sehemu ya mkakati wa kuboresha ubora wa huduma kwa kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika misimu iliyopita.
“Utalii ni biashara ya kimataifa, na kama hatutakuwa na ushindani wa kutosha, tutapoteza nafasi yetu sokoni.Hivyo ni lazima tuendelee kuboresha ubora wa huduma kila wakati,” alisema Maturo.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo pia ni jukwaa muhimu la wadau kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za kiutendaji hususan katika kipindi cha msimu wa chini wa utalii (low season), hali inayosaidia kuimarisha mikakati ya sekta hiyo.
Maturo amesisitiza kuwa TATO itaendelea kuandaa na kuratibu mafunzo kama haya, na pia inahitaji mafunzo hayo kupanuliwa kufika katika mikoa mingine nchini ili kuinua viwango vya huduma kitaifa.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ubora wa huduma ndiyo msingi mkuu wa ushindani wa Tanzania katika sekta ya utalii kimataifa, akibainisha kuwa wageni wanaokuja nchini wanapaswa kuondoka wakiwa mabalozi wazuri wa Tanzania duniani.
Ends .








0 Comments