WAZIRI MKUU AREJESHA MATUMAINI SOKO LA SIMU 2000 LILILOTEKEREA KWA MOTO DAR ES SALAAM

 MAAGIZO YA WAZIRI MKUU YAREJESHA MATUMAINI BAADA YA MOTO SIMU 2000

Na ArushaDigital | DAR ES SALAAM 


WAZIRI Mkuu, Mwigulu Nchemba, ameagiza hatua za dharura kuhakikisha shughuli za biashara zinarejea haraka kufuatia ajali ya moto ulioteketeza Soko la Mawasiliano maarufu kama Simu 2000, lililopo katika Kata ya Sinza, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Akiwa eneo la tukio Aprili 6, 2026 kukagua uharibifu mkubwa uliosababishwa na moto huo uliotokea Aprili 4, 2026, Waziri Mkuu alisema Serikali haitakaa kimya huku mamia ya wafanyabiashara wakipoteza mitaji yao, akisisitiza kuwa hatua za haraka na za vitendo zinapaswa kuchukuliwa kurejesha hali ya kawaida.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, takribani vibanda 500 viliteketea kwa moto huo, hali iliyowaacha wafanyabiashara wengi wakiwa katika sintofahamu kuhusu hatma ya biashara zao na maisha yao ya kila siku.

Akizungumza na waathirika hao, Dkt. Nchemba alitoa pole kwa niaba ya Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye tayari ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.

“Mheshimiwa Rais amepokea taarifa ya tukio hili na anawapa pole sana. Ameelekeza uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo cha tukio hili, na tayari kazi hiyo imeanza,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Katika kuhakikisha wafanyabiashara wanarejea haraka kwenye shughuli zao, Waziri Mkuu alitoa maagizo makali kwa uongozi wa Halmashauri ya Ubungo kuhakikisha eneo lote la soko linasafishwa ndani ya muda mfupi ili kutoa nafasi ya kuanza upya kwa biashara.

“Kesho eneo hili lote lisafishwe na kazi hiyo ikamilike kwa wakati ili wafanyabiashara waanze taratibu za kurejea,” aliamuru.

Mbali na hilo, Serikali imeahidi kushirikiana na taasisi za kifedha kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara waliopoteza mitaji yao, ikiwa ni pamoja na kurefusha muda wa marejesho ya mikopo waliyonayo na kuwezesha upatikanaji wa mikopo mipya yenye masharti nafuu kupitia mamlaka za serikali za mitaa.

Hatua hiyo inalenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa waathirika na kuwapa fursa ya kujikwamua kiuchumi kwa haraka.

Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kupanga upya miundombinu ya soko hilo, akitaka mpango wa ujenzi mpya kuzingatia uwepo wa eneo la stendi ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza ufanisi wa biashara.

Katika hatua nyingine, alikemea vikali vitendo vya ulanguzi wa vibanda vinavyojitokeza katika baadhi ya masoko, akisisitiza kuwa haki ya kupata kibanda ni ya wafanyabiashara halisi na si kwa walanguzi wanaotafuta faida kwa njia zisizo halali.

Waziri Mkuu pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akieleza kuwa mazingira ya amani ndiyo msingi mkuu wa ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ustawi wa jamii.

“Amani ni mtaji wa kila Mtanzania. Bila amani, hakuna biashara, hakuna maendeleo,” alisisitiza.

Akihitimisha, Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuthamini mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa taifa, akieleza kuwa sekta hiyo ndiyo injini kuu ya ajira na maendeleo kwa wananchi wengi.

Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu usalama wa masoko, miundombinu yake na umuhimu wa kuweka mifumo imara ya kinga dhidi ya majanga ya moto ili kuepusha hasara kubwa kama iliyotokea.




Ends .

Post a Comment

0 Comments