ISRAEL YAISHAMBULIA VIKUBWA VYA PETROKEMIKALI IRAN, YASEMA NI PIGO KUBWA KIUCHUMI
Na ArushaDigital
Mvutano wa kijeshi kati ya Israel na Iran umechukua sura mpya kufuatia mashambulizi makubwa yaliyolenga sekta muhimu ya uchumi wa Iran, huku Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, akitangaza kuharibiwa kwa vituo vikubwa vya petrokemikali.
Katika taarifa yake, Katz alisema vikosi vya jeshi la Israel (IDF) vimefanikiwa kushambulia moja ya vituo vikubwa zaidi vya uzalishaji wa kemikali za petroli nchini Iran kilichopo eneo la Asaluyeh, ambacho ni mhimili muhimu wa uzalishaji wa bidhaa za petrokemikali nchini humo.
Alieleza kuwa shambulio hilo ni sehemu ya operesheni pana ya kijeshi inayolenga kudhoofisha miundombinu ya kimkakati ya Iran, akisisitiza kuwa vikosi vya Israel vimepewa maagizo ya kuendelea kushambulia “kwa nguvu zote” ili kupunguza uwezo wa kiuchumi na kijeshi wa taifa hilo.
Kwa mujibu wa Katz, kituo hicho kilikuwa kinachangia sehemu kubwa ya uzalishaji wa petrokemikali wa Iran, huku akidai kuwa kwa pamoja na shambulio jingine lililofanywa wiki iliyopita dhidi ya kituo tofauti, sasa vituo viwili vikubwa vimeondolewa kabisa katika huduma.
“Taarifa zinaonesha kuwa vituo hivi viwili vilikuwa vinahusika na takribani asilimia 85 ya mauzo yote ya nje ya petrokemikali ya Iran. Kuviharibu ni pigo kubwa la kiuchumi lenye thamani ya makumi ya mabilioni ya dola,” alisisitiza Katz.
Aliongeza kuwa sekta ya petrokemikali ni uti wa mgongo wa uchumi wa Iran na chanzo kikuu cha fedha zinazodaiwa kufadhili shughuli za kijeshi pamoja na uimarishaji wa uwezo wa ulinzi wa taifa hilo.
Wakati huo huo, shirika la habari la Tasnim News Agency limethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo, likiripoti kuwa angalau kampuni mbili za petrokemikali zimeshambuliwa katika tukio hilo, ingawa halikutoa tathmini kamili ya uharibifu uliotokea.
Mashambulizi haya yanaongeza hofu ya kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, huku wachambuzi wa siasa wakionya kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri si tu uchumi wa Iran bali pia usalama wa nishati katika soko la dunia.
Hadi sasa, mamlaka za Iran hazijatoa taarifa rasmi kuhusu kiwango halisi cha uharibifu, lakini matarajio ni kuwa athari zake zinaweza kuwa kubwa kiuchumi na kisiasa, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inategemea kwa kiasi kikubwa bidhaa za nishati kutoka ukanda huo.

0 Comments