SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA UMEME ARUSHA, MKUDE AONYA MATUMIZI MABAYA YA MAGARI YA TANESCO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuimarisha huduma za nishati nchini baada ya kukabidhi vitendea kazi vipya kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Arusha, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kupunguza changamoto za umeme kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi za TANESCO mkoani hapa, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, alitoa onyo kali kwa watumishi dhidi ya matumizi mabaya ya magari hayo, akisisitiza kuwa ni mali ya umma inayopaswa kulindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mkude alisema serikali imetumia takribani shilingi bilioni 1.4 kununua magari hayo, yakiwemo yenye kreni, magari ya kiutendaji pamoja na bajaji, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za umeme mijini na vijijini.
“Rasilimali hizi zimegharimu fedha nyingi za walipa kodi, hivyo ni lazima zitumike kwa uadilifu mkubwa. Hatutavumilia matumizi yasiyo sahihi ya magari haya kwa maslahi binafsi,” alisisitiza Mkude.
Aliongeza kuwa ujio wa vitendea kazi hivyo utaiwezesha TANESCO kuongeza kasi ya kushughulikia hitilafu za umeme, kufikia maeneo ya pembezoni kwa urahisi na kuboresha huduma kwa wananchi kwa wakati.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Mhandisi Kisika Kisika, alisema upatikanaji wa magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha taasisi za umma zinapata vitendea kazi vya kutosha ili kuongeza ufanisi.
Alieleza kuwa Mkoa wa Arusha una hali nzuri ya upatikanaji wa umeme, ukipokea nishati kutoka vituo vitatu vikuu vya Njiro, Lemguru na Karatu, hali inayouweka mkoa huo katika nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji.
Hata hivyo, Kisika alibainisha kuwa matumizi ya umeme bado ni ya chini, ambapo mkoa unatumia takribani asilimia 30 tu ya umeme unaopatikana, huku zaidi ya asilimia 60 ikiwa ni ziada ambayo haijatumika.
“Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa Arusha bado ina fursa kubwa kwa wawekezaji, hususan katika sekta ya viwanda na biashara zinazohitaji nishati ya uhakika,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa mkoa una zaidi ya wateja laki tatu wa umeme, idadi inayoendelea kuongezeka kufuatia jitihada za serikali kusambaza huduma hiyo hadi vijijini na vitongoji.
Aidha, alisema karibu vijiji vyote mkoani humo tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku hatua zikichukuliwa kuhakikisha vitongoji vyote vinaunganishwa ili wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati hiyo muhimu.
Mkude aliipongeza TANESCO kwa kazi kubwa wanayoifanya, akisisitiza kuwa matumizi sahihi ya magari hayo yatakuwa chachu ya kuboresha zaidi huduma na kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi.
“Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya nishati kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi,” alisisitiza.
Uongozi wa TANESCO Mkoa wa Arusha uliahidi kuyatunza na kuyatumia ipasavyo magari hayo ili kuhakikisha yanaleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wateja.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, watumishi wa TANESCO pamoja na wadau wa sekta ya nishati, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu na huduma za umeme nchini.
Ends..















0 Comments