SHAMBULIO LA KUTISHA KANISANI UKEREWE: KIJANA AVAMIA IBADA YA PASAKA AKILENGA KUMUUA PAROKO, AUAWA NA WAUMINI

 SHAMBULIO LA KUTISHA KANISANI UKEREWE: KIJANA AVAMIA IBADA YA PASAKA AKILENGA KUMUUA PAROKO, AUAWA NA WAUMINI

Na ArushaDigital-UKEREWE|MWANZA

 Katika tukio la kushtua na kuzua hofu miongoni mwa waumini, kijana mmoja jana alivamia ibada ya Pasaka katika Parokia ya Bikira Maria Kagunguli, iliyopo wilayani Ukerewe, Jimbo Katoliki Bunda, akidaiwa kuwa na nia ya kumuua Paroko wa parokia hiyo, Fr. Arnold Bahati.

Tukio hilo lilitokea wakati ibada ikiendelea kwa utulivu, waumini wakiwa wameketi wakifuatilia ibada. Ghafla, kijana huyo alionekana akipanda ngazi kuelekea madhabahuni (Patakatifu), mahali alipokuwa Paroko Fr. Bahati, hali iliyozua taharuki ya ghafla kanisani.

Kwa mujibu wa mashuhuda, muumini mmoja aliyekuwa makini alimfuata haraka na kufanikiwa kumzuia kabla hajamfikia Paroko, akamtoa nje ya kanisa. Hata hivyo, baada ya kufika nje, kijana huyo alichomoa panga alilokuwa amelificha na kuanza kumshambulia muumini huyo kwa ukatili, akimjeruhi vibaya sehemu za mkono, kichwa na makalio.

Purukushani zilipozidi, waumini wengine walitoka nje kujaribu kuokoa hali, lakini mshambuliaji huyo aliwageukia na kuanza kuwashambulia kwa panga hilo. Katika vurugu hizo, muumini mwingine alijeruhiwa vibaya kwa kukatwakatwa sehemu mbalimbali za mwili.

Hata hivyo, kwa juhudi za pamoja, waumini walifanikiwa kumzidi nguvu mshambuliaji huyo na kumdhibiti. Katika sintofahamu hiyo, kijana huyo alipigwa na umati hadi kupoteza maisha.

Waumini waliojeruhiwa katika tukio hilo wamekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, huku hali zao zikielezwa kuwa mbaya lakini zinaendelea kufuatiliwa na madaktari.

Akizungumzia tukio hilo, Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda, Simon Masondele, alithibitisha kutokea kwake na kueleza kuwa si mara ya kwanza kwa kijana huyo kufanya jaribio la kumdhuru Paroko Fr. Bahati. Alisema kuwa katika tukio la awali, mshukiwa huyo aliwahi kuzuiwa na waumini kabla ya kutekeleza azma yake.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC) amethibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo na mazingira kamili ya tukio hilo. Taarifa za awali zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo anadaiwa kuwa na matatizo ya akili.

Tukio hilo limeacha simanzi, hofu na maswali mengi miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla, huku likizua mjadala kuhusu usalama katika maeneo ya ibada na umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya kikatili vinavyoweza kutokea ghafla.

Post a Comment

0 Comments