AFRICAN GALLERY YANG’ARA SEKTA YA UTALII KARATU ,SANAA YA MICHORO,PICHA NA VINYAGO YAWA KIVUTIO KWA WATALII, YAAJIRI ZAIDI YA WAFANYAKAZI 270,

AFRICAN GALLERY YANG’ARA SEKTA YA UTALII KARATU, YAAJIRI ZAIDI YA WAFANYAKAZI 270

Na Joseph Ngilisho | KARATU

KAMPUNI ya African Gallery iliyopo eneo la Manyara Kibaoni wilaya ya Karatu , mkoani Arusha, imeendelea kujijengea heshima kubwa kama kitovu cha biashara ya bidhaa za utalii nchini, huku ikitoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 270 na kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa ndani pamoja na maendeleo ya jamii.

Kampuni hiyo, inayofanya shughuli zake ndani ya eneo maarufu la Safari Land, imejikita katika uuzaji wa bidhaa mbalimbali zinazolenga soko la watalii, ikiwemo vinyago vya wanyama, vito vya thamani kama Tanzanite na mawe mengine ya thamani, pamoja na mavazi na kazi za sanaa zinazoakisi utamaduni wa Kiafrika.


Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Nishit Dodhia, alisema African Gallery si duka la kawaida bali ni kituo kikubwa cha ununuzi (shopping mall) kinachovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya kukuza utalii wa Tanzania kwa kutoa bidhaa bora na huduma za kipekee.

 Wageni wanaokuja hapa hupata nafasi ya kuona na kununua kazi za sanaa zinazobeba utambulisho halisi wa Afrika,” alisema Dodhia.

Aliongeza kuwa mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali yamechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa kampuni hiyo, huku yakivutia wawekezaji na kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii kwa ujumla.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Mauzo wa kampuni hiyo, Simon Samuel, alisema African Gallery ilianzishwa mwaka 2000 ikiwa na dhamira ya kuhudumia soko la utalii kupitia bidhaa za kipekee za sanaa, madini na kumbukumbu.

Alieleza kuwa watalii wengi wanaotembelea hifadhi za wanyama hupendelea kununua sanamu za wanyama waliowaona wakati wa safari zao, hali inayosaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.

“Mtalii anaponunua sanamu ya mnyama aliyemvutia na kuondoka nayo, anakuwa balozi wa utalii wetu nje ya nchi, kwa sababu watu wengine huuliza ilipotoka na kuvutiwa kuja Tanzania,” alisema Simon.

Mbali na mafanikio ya kibiashara, kampuni hiyo pia imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya jamii inayozunguka.

 Simon alibainisha kuwa African Gallery imefanikiwa kuanzisha shule ya msingi iliyokua kutoka wanafunzi 12 hadi zaidi ya 300 kwa sasa.

Aidha, kampuni hiyo imetekeleza miradi ya maji safi kwa kuchimba visima vitatu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo eneo la kampuni, shuleni pamoja na kijiji cha Soma wilayani Karatu, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

“Tunachokifanya si biashara pekee, bali pia ni kurudisha kwa jamii. Tunaamini maendeleo ya kweli yanapaswa kwenda sambamba na ustawi wa wananchi,” alisisitiza.

Katika kuhakikisha wageni wanapata uzoefu kamili, kituo hicho pia kinatoa huduma ya chakula na mapumziko kwa wasafiri wanaopita katika barabara ya Manyara kuelekea Karatu na maeneo mengine ya kitalii.

 

Naye mwongoza wageni wa kituo hicho, Venus Mwaliko, amewakaribisha watalii na wasafiri kutembelea African Gallery ili kujionea hazina ya sanaa na utamaduni wa Kiafrika.

“Hapa si sehemu ya kununua tu bidhaa, bali pia ni mahali pa kujifunza. Tunawaelezea wageni historia na maana ya kazi mbalimbali za sanaa zinazotengenezwa na wasanii wetu wa ndani,” alisema Mwaliko.

Aliongeza kuwa kituo hicho kinajivunia kuwa na mkusanyiko mkubwa wa sanaa, ikiwemo sanamu za mbao za Makonde, picha za wasanii wazawa, shanga za asili, pamoja na vitu vya kale (antiques) vyenye thamani ya kihistoria.

Kwa upande wa vito, alisema wanatoa madini ya kipekee kama Tanzanite inayopatikana Tanzania pekee, ikiwa imeundwa katika mapambo mbalimbali kama pete, mikufu na bangili kwa ajili ya kumbukumbu za wageni.

Kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya utalii na jamii, African Gallery inaendelea kuwa mfano wa mafanikio ya sekta binafsi nchini, ikionyesha jinsi biashara zinavyoweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi huku zikitangaza utamaduni wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

















Ends...


Post a Comment

0 Comments