SERIKALI YASIKIA KILIO CHA MBUNGE LUKUMAY BARABARA YA MBAUDA- OLJORO KUWEKWA LAMI,MBUNGE AMPONGEZA RAIS SAMIA, ASEMA SERIKALI YAKE SIKIVU..AOMBA TENA

  DKT. JOHANNES LUKUMAY AMPONGEZA RAIS SAMIA, AIBUKA NA NEEMA YA MIRADI ARUMERU MAGHARIBI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameibuka na kauli nzito ya matumaini kwa wananchi wake baada ya kueleza kwa kina mafanikio ya ziara na mawasiliano yake na Serikali Kuu, akimsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wenye usikivu na matokeo chanya kwa wananchi.

Akizungumza Katika ziara ya waziri Mkuu Mwiguli Nchemba katika hafla ya uzinduzi wa miradi ya barabara iliyofanyika Mbauda jijini Arusha, Dkt. Lukumay alisema alikutana na Rais Samia jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine alimpongeza kwa juhudi zake kubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini, akibainisha kuwa uwekezaji huo umeanza kuzaa matunda makubwa, hasa katika matibabu ya magonjwa sugu.

Alieleza kuwa Serikali imeongeza uwezo wa tiba nchini, ikiwemo matibabu ya saratani kupitia Taasisi ya Ocean Road Cancer Institute, pamoja na huduma za kibingwa katika magonjwa ya moyo, figo, kisukari na mifupa—hatua inayopunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi.

“Rais wetu ameonyesha dhamira ya kweli ya kuwajali Watanzania. Leo hii huduma za kibingwa zinapatikana hapa hapa nchini, jambo ambalo linapunguza gharama kwa wananchi na kuongeza uhai,” alisema Dkt. Lukumay kwa msisitizo.

Katika upande wa miundombinu, mbunge huyo alieleza kufurahishwa kwake na hatua ya Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuanza utekelezaji wa miradi muhimu ya barabara ndani ya jimbo lake, hasa ile ya kutoka Mbauda kupitia Oljoro hadi Losinyai—barabara ambayo imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi.

Alikumbusha kuwa wakati wa kampeni aliahidi kupigania ujenzi wa barabara hiyo, na sasa juhudi zake zimeanza kuzaa matunda baada ya Serikali kuonesha dhamira ya dhati ya kuitekeleza.

“Wananchi wa Oljoro walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri. Leo hii tunaona mwanga. Serikali imewasikia na sasa hatua zinaanza kuchukuliwa,baada ya waziri mkuu kuzindua ujenzi wa barabara ya Mbauda-Oljoro kwenda Losinyai ” alisema.




Dkt. Lukumay alisisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, hasa kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo, akibainisha kuwa ujio wa mashindano ya AFCON 2027 utatoa fursa kubwa zaidi kwa wananchi kunufaika kiuchumi iwapo miundombinu itaimarishwa kwa wakati.

Mbali na barabara hiyo, alitaja miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa kuwa ni pamoja na barabara za Malula–Bwawani, Loning'o–Seliani, Mangata–Sokoni 2, Kilimamoto–Mwandet, pamoja na Sambasha hadi Olmotonyi - Ngaramtoni, akisema zote zimepangwa katika mpango wa maendeleo na zimepata kipaumbele katika bajeti.

Alifichua kuwa ameishauri Serikali kuongeza fedha za dharura kwa ajili ya barabara kutoka shilingi bilioni 2.3 hadi kufikia bilioni 6 ili kukabiliana kwa haraka na changamoto zilizopo.

Katika hotuba yake, mbunge huyo pia aligusia mpango wa bima ya afya kwa wote, akieleza kuwa ni hatua ya kihistoria inayolenga kuwafikia wananchi wote, hasa makundi maalum kama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee na wasiojiweza.

Aliwataka wananchi kuendelea kuiamini Serikali yao, akisisitiza kuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na iko karibu na wananchi wake katika kusikiliza na kutatua changamoto zao.

“Serikali ya awamu ya sita ni sikivu na yenye vitendo. Wananchi wangu waendelee kuwa na imani, kudumisha amani na kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo,” alisisitiza Dkt. Lukumay.

Kwa ujumla, kauli ya mbunge huyo imeibua matumaini mapya kwa wananchi wa Arumeru Magharibi, wakiamini kuwa miradi hiyo itakapotekelezwa kikamilifu, itabadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya maisha na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.





Ends...

Post a Comment

0 Comments