POLISI ZANZIBAR WAMSHIKILIA MCHUMBA WA MAREHEMU ASHLY ROBINSON, UCHUNGUZI WAENDELEA ,A TO Z YA MCHUMBA WA KIMAREKANI KUJINYONGA HII HAPA.

 POLISI ZANZIBAR WAMSHIKILIA MCHUMBA WA MAREHEMU ASHLY ROBINSON, UCHUNGUZI WAENDELEA KUHUSU KIFO CHAKE

Na Arushadigital-ZANZIBAR

Jeshi la Polisi Visiwani Zanzibar linamshikilia raia wa kigeni, Joe McCann, ambaye ni mchumba wa marehemu Ashly Robinson maarufu kama “Ashlee Jenae”, kufuatia tukio la kifo chake lililotokea siku chache zilizopita baada ya kukutwa amejinyonga ndani ya chumba cha hoteli aliyofikia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 14, 2026, Naibu Kamishna wa Polisi Zanzibar ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Zuberi Chembera, amesema kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha kifo hicho. Amesema Jeshi la Polisi linashirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi huku mwili wa marehemu ukiendelea kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Lumumba, Mjini Unguja.

Kwa mujibu wa Chembera, taarifa za awali zinaeleza kuwa uongozi wa hoteli hiyo ulipokea malalamiko kutoka kwa mgeni aliyekuwa jirani na chumba namba 24, aliyedai kusikia malumbano kutoka chumba namba 25 ambacho kilikuwa kinatumiwa na marehemu pamoja na mchumba wake. Kutokana na hali hiyo, uongozi wa hoteli uliamua kumhamishia McCann katika chumba kingine namba 65, kilichopo umbali wa takribani dakika nane kwa miguu kutoka chumba cha awali.

Aidha, imeelezwa kuwa muda mfupi kabla ya tukio hilo, marehemu aliomba waya wa chaji kutoka kwa mfanyakazi wa hoteli kutokana na hitilafu ya waya wake. Mfanyakazi huyo alielekezwa kurejea baada ya dakika kumi, lakini aliporudi alimkuta marehemu akiwa amejitundika kwa kutumia kamba ya nguo. Juhudi za kuwahishwa hospitalini zilifanyika mara moja, lakini madaktari walithibitisha kuwa tayari alikuwa amefariki dunia.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa chanzo cha kifo hicho ni kukabwa. Chembera amesisitiza kuwa taarifa hizo si rasmi na hazijatolewa na mamlaka husika, hivyo amewataka wananchi kupuuza uvumi huo na kusubiri matokeo ya uchunguzi rasmi.

Ameongeza kuwa familia ya marehemu inaendelea kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa uchunguzi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa wawakilishi kutoka Taasisi ya Uchunguzi wa Vifo (Coroner), waliowasili kwa kibali cha ubalozi pamoja na ndugu wa familia.

Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa litatoa taarifa kamili mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Post a Comment

0 Comments