MAPENZI YAGEUKA MAUTI: RAIA WA MAREKANI AFARIKI UNGUJA, MPENZI WAKE AHOJIWA NA POLISI

 MAPENZI YAGEUKA MAUTI: RAIA WA MAREKANI AFARIKI UNGUJA, MPENZI WAKE AHOJIWA NA POLISI

Na Arushadigital|UNGUJA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja limetoa taarifa ya awali kuhusu tukio la kusikitisha la kifo cha raia wa Marekani, Ashly Robinson (31), likibainisha kuwa chanzo chake kinahusishwa na kutokuwepo kwa maelewano kati yake na mpenzi wake, Joseph Mccann.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, wawili hao walikuwa wamefikia katika hoteli moja visiwani humo, ambapo inadaiwa walikuwa wakikumbwa na migogoro ya kimapenzi iliyopelekea uongozi wa hoteli hiyo kuchukua hatua ya kuwatenganisha kwa kuwapatia vyumba tofauti, ili kudhibiti hali iliyokuwa imeanza kuonesha dalili za taharuki.

Inaelezwa kuwa licha ya hatua hiyo, hali haikutulia, na baadaye ndipo tukio hilo la kifo lilipotokea katika mazingira ambayo bado yanaendelea kuchunguzwa kwa kina na vyombo vya dola.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa hadi sasa Joseph Mccann anaendelea kushikiliwa kwa mahojiano zaidi, huku hati yake ya kusafiria ikizuiliwa ili kuzuia uwezekano wa kuondoka nchini kabla ya uchunguzi kukamilika.

Aidha, polisi wamesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea kwa umakini mkubwa ili kubaini ukweli kamili wa tukio hilo, ikiwemo kuchunguza ushahidi wa kitaalamu pamoja na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio.

Tukio hilo limeibua hisia miongoni mwa wakazi na wadau wa sekta ya utalii visiwani Zanzibar, huku likikumbusha umuhimu wa kushughulikia migogoro ya mahusiano kwa njia za amani ili kuepusha madhara makubwa kama haya.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa umma kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika pindi wanapokuwa na taarifa zozote zinazoweza kusaidia kukamilisha uchunguzi huo.

Ends..

Post a Comment

0 Comments