MBUNGE LUKUMAY AANDAA CHAKULA MAALUM KWA WATOTO YATIMA, AAHIDI KUENDELEA KUWASAIDIA; CCM YAMPONGEZA YAJIVUNIA KUMCHAGUA!

 MBUNGE LUKUMAY AANDAA CHAKULA MAALUM KWA WATOTO YATIMA, AAHIDI KUENDELEA KUWASAIDIA,CCM YAMPONGEZA YAJIVUNIA KUMCHAGUA

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, ameendelea kudhihirisha moyo wa upendo na kujali jamii baada ya kuwaandalia chakula maalum watoto yatima wanaotoka katika kituo cha malezi, katika hafla iliyofanyika nyumbani kwake, Kata ya Kiranyi.

Hafla hiyo iliyojaa furaha na upendo iliwakutanisha watoto hao pamoja na wadau mbalimbali, huku Dkt. Lukumay akieleza kuwa tukio hilo ni sehemu ya shukrani zake kwa Mwenyezi Mungu na dhamira yake ya dhati ya kuendelea kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa leo. Pia nampongeza Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hususan watoto wenye uhitaji maalum,” alisema Lukumay.

Mbunge huyo alieleza kuwa familia yake imekuwa nguzo muhimu katika safari yake ya kisiasa na kijamii, akimpongeza mke wake kwa mchango wake wa kiroho na kimaadili unaompa nguvu ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Aidha, aliwapongeza viongozi wa dini na wananchi wanaoendelea kumuombea na kumpa ushirikiano, akisisitiza kuwa mchango wao unaimarisha uwezo wake wa kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia umuhimu wa tukio hilo, Dkt. Lukumay alisema ni ishara ya upendo na faraja kwa watoto yatima, akibainisha kuwa watoto hao wanahitaji malezi bora, msaada na mazingira rafiki yatakayowawezesha kufikia ndoto zao.

Kwa upande wao, walezi wa kituo cha watoto yatima walimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo, wakisema umeleta faraja kubwa na kuongeza matumaini kwa watoto hao.

Watoto walionekana kufurahia tukio hilo kwa kushiriki nyimbo, michezo na burudani mbalimbali, huku wakionesha shukrani zao kwa mbunge huyo na familia yake kwa kuwajali na kuwakaribisha nyumbani kwake.

Akihitimisha, Dkt. Lukumay aliahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha maisha ya watoto yatima na makundi mengine yenye uhitaji maalum.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kimnyaki, Godson Mollel, alimpongeza mbunge huyo kwa kitendo chake cha kujitoa kwa jamii, akisema ni mfano wa uongozi bora unaopaswa kuigwa.

Mollel alisema chama pamoja na wananchi wa Kata ya Kimnyaki wanajivunia uongozi wa Dkt. Lukumay, akimtaja kuwa ni kiongozi anayejali makundi maalum na kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wake.

“Tunakupongeza Mheshimiwa Mbunge kwa moyo wako wa kujali jamii, hususan watoto yatima. Huu ni mfano wa uongozi unaoonesha upendo, mshikamano na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi,” alisema Mollel.


Ends..

Post a Comment

0 Comments