By ArushaDigital
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya siku tatu kuhusu uwezekano wa mvua kubwa zitakazoweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani, ikiwemo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne Aprili 7, 2026, mvua hizo zinatarajiwa kuanza kesho Jumatano na kuendelea hadi Ijumaa, zikiathiri pia mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga na Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika taarifa hiyo, TMA imebainisha kuwa uwezekano wa mvua hizo pamoja na athari zake uko katika kiwango cha kati, lakini bado kuna hatari ya kutokea kwa mafuriko katika baadhi ya maeneo. Hali hii inaweza kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hususan katika maeneo yenye miundombinu hafifu au yaliyo katika mabonde.
Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari mapema, ikiwa ni pamoja na kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, kuepuka maeneo hatarishi na kuhakikisha wanachukua hatua za kujikinga dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

إرسال تعليق