IJUMAA KUU ARUSHA: HOTAY, MKUDE WAHUBIRI MSAMAHA, UPENDO NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWENYEKITI wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Arusha (UKAMA), Askofu Dkt. Stanley Hotay, amewataka Watanzania kutambua kuwa Ijumaa Kuu si tukio la kihistoria pekee, bali ni siku yenye ujumbe hai wa msamaha, upendo na mabadiliko ya maisha.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, malezi bora na mshikamano wa kijamii.
Viongozi hao walitoa wito huo wakati wa ibada ya pamoja ya madhehebu mbalimbali ya Kikristo iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa Katoliki Mtakatifu Thereza, Jimbo Kuu la Arusha, iliyohudhuriwa na mamia ya waumini.
Akihubiri, Askofu Hotay alisema msalaba wa Yesu Kristo una maana pana zaidi ya mateso, kwani ndio chanzo cha msamaha na ukombozi wa mwanadamu.
Alieleza kuwa licha ya kunyanyaswa, kutukanwa na kudhalilishwa, Yesu alichagua kusamehe badala ya kulipiza kisasi, akitoa mfano wa hali ya juu wa uvumilivu na upendo.
“Watu wengi husema wokovu ni bure, lakini ukweli ni kwamba ulilipiwa gharama kubwa sana. Yesu aliteseka kwa ajili yetu, akitufundisha thamani ya kusamehe,” alisema.
Askofu Hotay alikumbusha pia tukio la Yesu kufunga siku 40 jangwani, akisema hata alipokumbwa na njaa kali, alikataa majaribu ya kugeuza mawe kuwa mkate, akichagua kumtii Mungu badala ya tamaa za mwili. Alisema ushindi huo unaonesha kuwa nguvu ya kiroho inaweza kushinda changamoto za maisha.
Akifafanua zaidi, alisema msalaba ni mahali ambapo msamaha wa mwanadamu ulizaliwa na kwamba ndani yake ndipo kunapatikana nguvu ya kusamehe hata pale inapokuwa vigumu.
Aidha, aliwataka Watanzania kutumia maadhimisho ya Ijumaa Kuu kujitathmini binafsi na kitaifa, akionya kuwa jamii imejaa majeraha ya kifamilia, kijamii na kibiashara yanayohitaji uponyaji kupitia msamaha.
“Watu wengi wanaishi katika vifungo visivyoonekana kwa sababu ya kutokusamehe. Kutokusamehe humuumiza zaidi anayebeba chuki kuliko aliyekosewa,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alisisitiza kuwa maadhimisho ya Ijumaa Kuu yanapaswa kuwa chachu ya kujenga jamii yenye huruma, maadili mema na mshikamano.
“Ijumaa Kuu inatukumbusha umuhimu wa sadaka, upendo na kusameheana. Tunapaswa kuyatafsiri mafunzo haya katika maisha yetu ya kila siku, hasa katika malezi ya watoto wetu,” alisema Mkude.
Alieleza kuwa malezi bora kwa watoto na vijana ni msingi wa taifa lenye ustawi, akiwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanajenga misingi ya heshima, utii na uwajibikaji kwa kizazi kijacho.
Mkude aliongeza kuwa wakati Arusha ikijiandaa kupokea wageni wa kimataifa kuelekea michezo ya AFCON 2027, wananchi wanapaswa kujijengea tabia ya ukarimu, nidhamu na kuzingatia usafi wa mazingira ili kulinda taswira ya jiji hilo.
Pia aliwahimiza viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na mshikamano, akibainisha kuwa dini zina mchango mkubwa katika kuijenga jamii yenye utulivu na maadili.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kuendeleza utamaduni wa kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuendelea kuiombea nchi pamoja na viongozi wake wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Ikiwa tutasimama pamoja katika upendo na amani, Arusha itakuwa mfano wa kuigwa si tu nchini bali hata kimataifa,” alisisitiza.
Ibada hiyo ya Ijumaa Kuu ilihitimishwa kwa sala maalum za kuiombea nchi, viongozi wake na kudumisha amani ya taifa, huku ikionesha mshikamano mkubwa wa Wakristo wa madhehebu mbalimbali katika kuadhimisha mateso na kifo cha Yesu Kristo.
ENDS













0 Comments