JOWUTA Kutoa Tuzo kwa Wanahabari Bora Mei Mosi
Na Joseph Ngilisho| Arushadigital, Dodoma
CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimetangaza mpango wa kutoa tuzo na zawadi kwa wafanyakazi bora katika sekta ya habari, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yatakayofanyika kitaifa mkoani Njombe mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma Siwayombe, amesema hatua hiyo inalenga kutambua na kuthamini mchango wa wanahabari katika kuhabarisha umma na kuchochea maendeleo ya taifa.
Amesema mwaka huu ni wa kipekee kwa JOWUTA kushiriki rasmi maadhimisho ya Mei Mosi kwa mara ya kwanza, tangu chama hicho kilipojiunga na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mwaka jana.
Kwa mujibu wa Siwayombe, JOWUTA ilipata uanachama wa TUCTA katika maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika mkoani Singida mwaka 2025, tukio lililohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, baada ya chama hicho kukidhi vigezo vyote vya kujiunga na shirikisho hilo.
“Kwa mara ya kwanza, tutatoa tuzo kwa wafanyakazi bora katika vyombo vya habari katika ngazi ya kitaifa na baadhi ya mikoa. Tayari mchakato wa kuwatambua umeanza,” amesema Siwayombe.
Amefafanua kuwa uamuzi huo umetokana na azimio la Kamati ya Utendaji ya JOWUTA, kwa lengo la kuhamasisha ubora wa kazi na kutambua juhudi za wanahabari wanaotekeleza majukumu yao licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali kazini.
“Tunao wanachama zaidi ya 500 nchi nzima ambao wanafanya kazi kubwa ya kuhabarisha jamii kuhusu masuala ya maendeleo. Ni muhimu mchango wao ukatambuliwa na kuthaminiwa,” ameongeza.
Aidha, Siwayombe ameiomba Serikali, mashirika ya umma na sekta binafsi kujitokeza kudhamini tuzo hizo, akieleza kuwa hatua hiyo itachochea ari ya utendaji bora miongoni mwa wanahabari.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, amesema chama hicho tayari kimewasilisha maombi ya ufadhili kwa taasisi mbalimbali zinazoshirikiana na vyombo vya habari.
Amesema ni wakati muafaka kwa wanahabari kutambuliwa sawa na kada nyingine za wafanyakazi kama walimu, madaktari na sekta binafsi, ambao wamekuwa wakipatiwa tuzo kila mwaka.
“Tunaamini wadau mbalimbali watajitokeza kuunga mkono jitihada hizi ili kuhakikisha wanahabari bora wanatambuliwa na kupewa motisha stahiki,” amesema Msuya.
JOWUTA pia imewataka wanahabari nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mei Mosi na kutumia fursa hiyo kuibua mijadala inayolenga kuboresha mazingira ya kazi, ikiwemo haki za msingi kama mikataba ya ajira na stahili nyingine.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu ni: “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”
Ends




0 Comments