DC DKT. KARANGA AFUNGUA RASMI SHUGHULI ZA UVUVI ZIWA EYASI BAADA YA UTAFITI, AONYA UVUVI HARAMU

 Na Joseph Ngilisho | KARATU

Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dkt. Lameck Karanga, ametangaza rasmi kufunguliwa kwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Eyasi, zilizokuwa zimesitishwa kwa muda kupisha zoezi la utafiti wa kitaalamu uliolenga kubaini hali halisi ya rasilimali za samaki na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji endelevu.

Akizungumza Aprili 16, 2026 katika kijiji cha Mang’ola mbele ya wananchi, wavuvi na viongozi mbalimbali, Dkt. Karanga alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya majadiliano ya kina yaliyohusisha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, viongozi wa vijiji vinavyozunguka ziwa hilo, wataalamu wa uvuvi kutoka Halmashauri pamoja na wadau wakuu wa sekta hiyo.


Alieleza kuwa kikao hicho kiliridhia kwa pamoja kurejesha shughuli za uvuvi katika bonde la Ziwa Eyasi, huku kikisisitiza umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zote za uvuvi ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


“Serikali ilisimamisha shughuli hizi kwa nia njema ya kufanya utafiti na kupanga matumizi bora ya rasilimali za ziwa. Sasa tumefikia hatua ya kuruhusu shughuli kuanza tena, lakini kwa masharti ya nidhamu na ufuatiliaji wa karibu,” alisema Dkt. Karanga.


Hata hivyo, alionya vikali dhidi ya vitendo vya uvuvi haramu vinavyofanywa na baadhi ya watu, akiwemo wahamiaji kutoka mataifa jirani, ambao wamekuwa wakivua bila kufuata sheria na kuhatarisha uhai wa samaki pamoja na uchumi wa wananchi wa eneo hilo.


Alisisitiza kuwa vyombo vya dola vitachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na uvuvi haramu, akibainisha kuwa ulinzi wa rasilimali za taifa ni jukumu la kila mwananchi.


Kwa upande wao, wananchi wa Mang’ola na maeneo jirani walipokea kwa shangwe uamuzi huo, wakisema umerejesha matumaini ya kipato baada ya kipindi kigumu walichokumbana nacho kufuatia kusitishwa kwa shughuli za uvuvi.


Baadhi ya wavuvi walieleza kuwa kurejea kwa shughuli hizo kutasaidia kuimarisha uchumi wa kaya nyingi zinazotegemea ziwa hilo, huku wakiahidi kushirikiana na Serikali katika kulinda rasilimali hiyo muhimu.


Kufunguliwa kwa uvuvi katika Ziwa Eyasi kunatarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Karatu pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka ziwa hilo. 


Serikali imeeleza kuwa itaendelea kufanya mashauriano na wadau mbalimbali ili kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa uvuvi, utakaozuia migogoro na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa manufaa ya taifa.





Ends..

Post a Comment

0 Comments