BILIONI 525 ZALETA NEEMA YA MAJI ARUMERU MAGHARIBI,MBUNGE LUKUMAY AKABIDHIWA MTANDAO WA MABOMBA YA MAJI YA MRADI WA BILIONI 2.7, CCM YAMPONGEZA AIBUKA SHUJAA WA MAENDELEO ANAYEAHIDI NA KUTEKELEZA!

BILIONI 525 ZALETA MAPINDUZI YA MAJI ARUMERU MAGHARIBI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amepokea rasmi mabomba ya mradi mkubwa wa maji wa Jiji la Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 525, hatua ambayo imeelezwa kuwa mkombozi kwa wananchi wa kata za Kimnyaki, Tarakwa, Siwandeti, Kiranyi, Olorien na maeneo jirani.

Hafla ya kukabidhi mabomba hayo imefanyika katika Kitongoji cha Siwandeti, Kata ya Kiranyi, ambapo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) ilikabidhi miundombinu hiyo kwa mbunge kwa niaba ya wananchi watakaonufaika.

Dkt. Lukumay alisema mradi huo ni suluhisho la muda mrefu la changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa utekelezaji wa ahadi ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata maji karibu na makazi yake.

“Hatua hii ya kukabidhi mabomba ni mwanzo wa utekelezaji wa vitendo wa ahadi ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anapata maji karibu na makazi yake,” alisema Dkt. Lukumay.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan, imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya maji ili kuondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi. Aidha, aliwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo muhimu ili iweze kudumu na kuendelea kuwanufaisha, huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni nguzo ya mafanikio ya miradi ya maendeleo.

Wananchi wa maeneo ya Kimnyaki, Tarakwa, Siwandeti na Olorieni tayari wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kufuatia utekelezaji wa mradi huu unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.7.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Kanda ya Ngaramtoni, Mhandisi Ansila Temu, alisema mabomba yaliyokabidhiwa yana urefu wa kilomita 4.5 na ukubwa wa nchi tatu, yakilenga kuendeleza mradi unaohudumia maeneo hayo. Mradi mzima una urefu wa kilomita 67 na unalenga kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa urahisi na usalama.

“Hadi sasa mabomba yenye urefu wa kilomita 8.5 yameshalazwa, huku kazi ikiendelea katika maeneo mbalimbali ili kukamilisha mradi kwa wakati. Katika maeneo ambayo tayari kazi imekamilika, wananchi wameanza kupata huduma ya maji kupitia vituo maalum vya kuchotea maji, ambapo vituo 17 tayari vimefunguliwa katika eneo la Kimnyaki,” alisema Mhandisi Temu.

LUKUMAY APEWA PONGEZI !

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Baraka Simion, amempongeza Dkt. Lukumay kwa juhudi zake za kufanikisha mradi huu, huku akitumia jukwaa hilo kuwasilisha changamoto zinazolikabili jimbo hilo.

Simion alisema baadhi ya maeneo bado yanakabiliwa na tatizo la maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya fluoride, hasa ukanda wa Oldonyowasi na Oldonyosambu, na kuhitaji kipaumbele cha haraka. Pia alibainisha changamoto za miundombinu ya barabara, zikihitaji uboreshaji haraka ili kuendeleza shughuli za kiuchumi.

“Tunatambua kazi nzuri inayoendelea, lakini bado tunaomba nguvu zaidi iongezwe katika miundombinu ya barabara ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wetu,” alisema Simion.

Barabara zilizotajwa ni pamoja na Malula – Nduruma – Bwawani, Sokon II – Bangata, pamoja na barabara nyingine za vijijini zinazoelekea Kiterai na maeneo jirani.

Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza matumaini yao makubwa kwa mradi huu, wakisema utasaidia kupunguza mateso ya muda mrefu ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

CCM YAPONGEZA MBUNGE WA ARUMERU MAGHARIBI

Katibu wa Siasa na Ujenzi wa CCM katika Halmashauri ya Arusha DC, Nicolaus Sawa, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa serikali na wabunge, akimpongeza Dkt. Lukumay kwa jitihada zake za kuhakikisha kata zinazopitiwa na mradi wa bilioni 525 zinanufaika moja kwa moja.

“Hii ni ishara ya wazi ya jinsi CCM inavyoweka mbele ustawi wa wananchi. Mabomba haya ni mfano halisi wa matokeo yanayopatikana pale tunaposhirikiana kwa busara na uzalendo,” alisema Sawa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wananchi, na wajumbe wa CCM, wote wakiangazia faida za mradi unaoendelea kuwanufaisha wakazi wa Arumeru Magharibi na maeneo jirani.

Mradi huu unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za serikali ya Awamu ya Sita kuboresha huduma za kijamii nchini, huku ukitarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa maelfu ya wananchi wa kata za jimbo hilo.














Ends..

Post a Comment

0 Comments