Basi la Abood lakamatwa na mirungi kilo 101.2 Dar, DCEA yafichua mtandao mpana wa usafirishaji
By Arushadigital
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 101.2 zilizokuwa zimefichwa kwa ustadi ndani ya basi la abiria la kampuni ya Abood, katika eneo la Tabata Kibo jijini Dar es Salaam.
Basi hilo aina ya Yutong lenye namba ya usajili T 181 EMJ lilikuwa likifanya safari zake kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania, likitumiwa kama njia ya kusafirisha dawa hizo haramu bila kubainika kirahisi.
Akizungumza Aprili 14, 2026, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mirungi hiyo ilikuwa imefichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo, ikiwemo ndani ya mfumo wa kiyoyozi (AC), ikiwa ni mbinu ya kukwepa ukaguzi wa kawaida.
Katika operesheni hiyo, watu watano walikamatwa akiwemo dereva wa basi hilo, Ramadhan Mohamed (52), pamoja na kondakta Salma Sanga (26). Wengine ni Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39), ambao wote wanashikiliwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Lyimo alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria, wahusika wakuu wanaokamatwa katika matukio kama hayo ni wale wanaokutwa moja kwa moja na mzigo husika, hali iliyosababisha basi hilo pia kushikiliwa kama kielelezo muhimu cha ushahidi.
Katika tukio lingine mkoani Pwani, DCEA ilikamata kilogramu 419.09 za mirungi zilizokuwa zikisafirishwa kuelekea Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya operesheni kubwa ya kitaifa ya kudhibiti biashara hiyo haramu.
Akitoa tathmini ya operesheni zilizofanyika nchi nzima, Lyimo alisema mamlaka hiyo imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, pamoja na kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu. Pia, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa.
Aidha, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na watuhumiwa 77 kukamatwa, huku vyombo vya usafiri vikiwemo magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vikikamatwa katika operesheni hizo.
Uchambuzi wa takwimu unaonyesha kuwa mirungi imeendelea kuongoza kwa wingi wa ukamataji, ambapo kilogramu 1,267.12 sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi husika ni aina hiyo.
“Hii inatokana na mkakati wetu wa kuelekeza nguvu zaidi katika operesheni za mashambani baada ya kudhibiti kwa kiwango kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani,” alisisitiza Lyimo.
Katika matukio mengine, mkoani Mwanza, kilogramu 52 za mirungi zilikamatwa katika kizuizi cha barabarani cha Magu na Bandari ya Mwanza South, zikiwa zimefichwa ndani ya gari aina ya Fuso (T 296 APA) katikati ya mizigo ya nguo za mitumba. Dereva wake, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana, alikamatwa.
Wilayani Misungwi, mkoani humo, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa nyumbani kwa wanandoa Chrispin Shoo (62) na Esther Pastory (55), pamoja na magari mawili—Toyota Crown (T 742 EGL) na Toyota Wish (T 854 DXB)—na bajaji (MC 261 EZV).
Mkoani Tanga, DCEA ilikamata kilogramu 32.95 za mirungi zilizokuwa zimechanganywa na maembe ndani ya mfuko, huku mtuhumiwa Seif Omar (38), maarufu kama Haniwao, akitiwa mbaroni. Operesheni nyingine mkoani humo zilinasa jumla ya kilogramu 164.01 za mirungi katika matukio tofauti.
Operesheni hizi zinaonesha kuimarika kwa mikakati ya DCEA katika kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya nchini, huku mamlaka hiyo ikiendelea kuonya wahusika kuacha mara moja vitendo hivyo vinavyohatarisha usalama na afya ya jamii.
NB:Picha ya Basi lililokamatwa siyo iliyopo kwenye story hii ila ni kama hilo la kampuni hiyo.
Ends..


0 Comments