WAZIRI ALIYEJITEKA KUKWEPA MADENI AKAMATWA

 TUJU AKAMATWA, DCI YASEMA ALIJIFICHA NYUMBANI BADALA YA KUTEKWA

Na ArushaDigital | Kenya


Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya (DCI) imemtia mbaroni aliyekuwa Waziri wa zamani wa nchi hiyo, Raphael Tuju, kufuatia kile kinachoelezwa kuwa ni kutoa taarifa za kupotosha kuhusu madai ya kutekwa kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa DCI, Amin Mohamed, alisema uchunguzi wa kina wa kitaalamu umebaini kuwa Tuju hakuwa ametekwa kama ilivyoripotiwa awali, bali alikuwa amejificha nyumbani kwake muda wote.

Kwa mujibu wa DCI, mara baada ya kuripotiwa kupotea Jumamosi, maafisa walianza uchunguzi wa haraka kufuatilia tukio hilo. Hata hivyo, jitihada hizo zilikwamishwa na familia ya Tuju kuwazuia baadhi ya maafisa kuingia nyumbani kwake eneo la Karen, hatua iliyoongeza mashaka na kulazimu polisi kuzingira eneo hilo wakisubiri kibali cha mahakama kufanya upekuzi.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa uchunguzi wa mienendo yake, ikiwemo ufuatiliaji wa mawasiliano, ulionyesha wazi kuwa Tuju alikuwa nyumbani hata baada ya simu yake kuzimwa.

DCI ilisema Tuju aliamua kujitokeza mwenyewe baada ya kubaini kuwa ukweli ulikuwa ukianza kufichuka. Polisi wanamtuhumu kwa kupanga tukio la utekaji kwa lengo la kupotosha umma, wakisisitiza kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la jinai.

Hata hivyo, kwa upande wake Tuju alikanusha madai hayo akidai kuwa alilazimika kujificha baada ya kuhisi anafuatiliwa na gari lisilo na namba za usajili. Alieleza kuwa alifanikiwa kuwakwepa waliokuwa wakimfuatilia kwa kubadili njia mara kadhaa kabla ya kuliacha gari lake katika eneo la Miotoni Lane, Karen, na kwenda kujificha.

Aidha, alidai kuwa aliwajulisha polisi kuhusu tukio hilo na kuchukua hatua za tahadhari kwa kuhofia usalama wake.

Awali, familia ya Tuju iliripoti kupotea kwake ikidai kuwa alikuwa akisafiri pamoja na dereva wake kuelekea kwenye mahojiano ya redio, tukio lililozua taharuki kubwa na maswali kuhusu usalama wake kabla ya kujitokeza kwake hadharani.

Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea huku mamlaka zikisisitiza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayebainika kutoa taarifa za uongo.

Post a Comment

0 Comments