WAKAZI ZAIDI YA 300 LOLIONDO WALIA KUFA NJAA, DC AONGOZA KUFYEKA MAZAO – CCM YALIPUKA , MBUNGE ATAKA WANANCHI WALIPWE FIDIA YA HARAKA,DC AGOMA KUPOKEA SIKU WIKI NZIMA,TIZAMA PICHA UTALIA!

 WAKAZI LOLIONDO WALIA NJAA, DC AONGOZA KUFYEKA MAZAO – CCM YALIPUKA, MBUNGE ATAKA FIDIA YA HARAKA

Na Joseph Ngilisho | NGORONGORO

 

HALI ya sintofahamu imeikumba Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha baada ya mamia ya wakazi wa Loliondo kulalamikia uharibifu wa mazao yao unaodaiwa kufanywa na uongozi wa wilaya chini ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, tukio linalotajwa kusababisha hofu kubwa ya baa la njaa kwa familia nyingi.

Wakazi hao wanadai kuwa zoezi hilo lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, lilifanyika bila taarifa wala ushirikishwaji wa wananchi, huku mashamba ya mahindi yenye takribani hekari 70 yakifyekwa katika hatua ambayo wengi wanasema imewaacha bila matumaini ya chakula wala kipato.


Akizungumza kwa masikitiko, mmoja wa wakulima walioathirika, Seduga Peter Msuya, alisema hatua hiyo imewaumiza sana kwani mazao yao yalikuwa tayari yameanza kubeba na yalitegemewa kuokoa familia zao kiuchumi.

“Tunashangaa kuona mazao yetu yakifyekwa ghafla bila hata maelezo. Hatukushirikishwa kabisa. Haya ni mashamba ya urithi wa familia zetu tangu miaka ya nyuma,” alisema Msuya.

Kwa mujibu wa wakazi hao, maeneo hayo yamekuwa yakitumika kwa kilimo tangu miaka ya 1970 na 1980, ingawa matumizi yake yalianza kuongezeka zaidi tangu mwaka 2012 baada ya changamoto za wanyama wakali kupungua.

Hata hivyo, mamlaka zinadaiwa kueleza kuwa wananchi hao walikuwa wakilima katika maeneo tengefu, jambo ambalo wakazi wanakiri kulifahamu lakini wanasisitiza kuwa walipaswa kupewa elimu na muda wa kujiandaa badala ya hatua ya ghafla ya kuharibu mazao yao.

KILIO CHA WANANCHI: “TUTAKULA NINI?”

Kwa upande wake, Sophia Lulu, mkazi mwingine wa Loliondo, alisema amepata hasara kubwa baada ya shamba lake kufyekwa huku mahindi yakiwa tayari yamechanua.

“Nilikuwa nategemea mavuno haya kwa familia yangu. Sasa hatuna chakula, hatujui tutaishi vipi. Tunaomba msaada wa haraka,” alisema kwa huzuni.

Wakazi wengi sasa wanaiomba serikali kuanzia ngazi ya juu kuingilia kati haraka ili kunusuru maisha yao, wakihofia kuwa bila msaada wa dharura, eneo hilo linaweza kukumbwa na baa kubwa la njaa.

CCM YACHUKUA HATUA, YAPELEKA MALALAMIKO TAIFA

Katika hatua nyingine iliyozua mjadala mkubwa wa kisiasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngorongoro kimejitokeza kulaani vikali tukio hilo, kikidai halikushirikishwa katika uamuzi huo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo, Lucas Masiaya, alisema kitendo hicho kinakiuka misingi ya uwajibikaji na ushirikishwaji.

“Hiki ni kitendo kisichokubalika. CCM tunalaani vikali hatua hii na tayari tumeshapeleka taarifa ngazi ya mkoa na taifa ili haki za wananchi zilindwe,” alisema Masiaya.

Taarifa hiyo imefikishwa hadi ngazi za juu za chama, ambapo imesisitizwa kuwa haki za wananchi lazima ziheshimiwe na taratibu zifuatwe kabla ya kuchukua hatua kama hizo.

MBUNGE ATOA MSIMAMO MKALI, ADAI FIDIA

Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, naye ameibuka na msimamo mkali akilaani tukio hilo na kulitaja kuwa ni kinyume cha haki za binadamu.

“Wananchi hawa walikuwa wanategemea mazao haya kwa maisha yao. Wengine walishayaweka dhamana kupata mikopo ya kusomesha watoto. Leo wameachwa bila kitu,” alisema Ndoinyo.

Mbunge huyo ameishinikiza serikali kuchukua hatua za haraka ikiwa ni pamoja na,Kutoa msaada wa chakula kwa wananchi walioathirika,Kulipa fidia kwa mazao yote yaliyoharibiwa,Kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa

“Haiwezekani wananchi waachwe wakifa njaa kutokana na maamuzi yasiyozingatia utu na haki,” alisisitiza.

DC HAPATIKANI, RAS NA MKURUGENZI WAJITOA

 
DC SAKULO- Ngorongoro 

Katika jitihada za kupata upande wa pili wa taarifa hii, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, alitafutwa kwa njia ya simu bila mafanikio, ambapo kwa takribani wiki moja hakuweza kupokea simu zake.

Pia, ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) ulitumwa mara kadhaa kuomba ushirikiano wake ili kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma zinazomkabili, hata hivyo hakujibu chochote hadi wakati wa kuchapishwa kwa habari hii. Jitihada za kumpata zinaendelea.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Hamza Hamza, alipotafutwa alisema suala hilo linapaswa kuzungumzwa na Mkuu wa Wilaya mwenyewe, akimaanisha kuwa yeye hana mamlaka ya kulizungumzia kwa kina.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Murtallah Sadiq Mbilu, alisema amepata taarifa za tukio hilo lakini akasisitiza kuwa ofisi yake haihusiki moja kwa moja na zoezi hilo.

“Nimelisikia jambo hilo, lakini ofisi yangu haihusiki. Anayepaswa kulizungumzia ni Mkuu wa Wilaya. Mimi kwa sasa nipo Dodoma, na siku tukio linatokea nilikuwa safarini,” alisema Mbilu.

HOFU YA NJAA YATAWALA

Taarifa zinaeleza kuwa zaidi ya kaya 70 zimeathirika moja kwa moja na tukio hilo, huku wengi wakikiri kuwa walitegemea mavuno hayo kwa mahitaji muhimu ya maisha ikiwemo chakula, ada za shule na huduma za msingi.

Kwa sasa, Loliondo imegeuka kuwa kitovu cha mjadala mzito kati ya wananchi, viongozi wa serikali na wanasiasa, huku swali kubwa likibaki: nani atawajibika kwa hasara hii na lini msaada utawafikia wananchi?

Wakati macho ya wengi yakielekezwa serikalini, wakazi wa Loliondo wanaendelea kusubiri majibu—wakihofia kuwa bila hatua za haraka, kilio chao cha leo kinaweza kuwa janga la kesho.













Ends..

Post a Comment

0 Comments