VIONGOZI AFYA WANOLEWA USIMAMIZI WA CHANJO, SERIKALI YALENGA KUMFIKIA KILA MTOTO

 VIONGOZI AFYA WANOLEWA USIMAMIZI WA CHANJO, SERIKALI YALENGA KUMFIKIA KILA MTOTO

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imeanza hatua mpya ya kuimarisha huduma za chanjo nchini kwa kuwajengea uwezo viongozi wa sekta ya afya, kwa lengo la kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki hiyo muhimu ya msingi.

Hatua hiyo inatekelezwa kupitia mafunzo maalum ya siku tano yanayoendelea jijini Arusha chini ya Mpango wa Taifa wa Chanjo, yakiwakutanisha waganga wakuu wa mikoa, waganga wakuu wa halmashauri pamoja na makatibu wa afya kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa Afya Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo, Bonaventure Nestor, alisema lengo kuu ni kuwaimarisha viongozi hao ili waweze kusimamia kwa ufanisi utoaji wa huduma za chanjo kuanzia ngazi ya mkoa hadi jamii.

Alisema serikali imepiga hatua kubwa ambapo kiwango cha utoaji wa chanjo kimefikia zaidi ya asilimia 98, lakini bado kuna changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja, ikiwemo kuwafikia watoto wanaoishi katika maeneo ya pembezoni na yenye mazingira magumu.

“Tunataka kuona kila kiongozi anakuwa na uelewa wa kina wa kusimamia huduma za chanjo ili kuhakikisha zinawafikia walengwa wote kwa wakati na ubora unaotakiwa,” alisema Nestor.

Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna baadhi ya maeneo yanayokumbwa na changamoto za usambazaji wa chanjo, uhifadhi pamoja na uelewa mdogo wa jamii, hali inayosababisha baadhi ya watoto kukosa huduma kwa wakati.


Kwa upande wake, Afisa wa Chanjo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Rosaria Arope, alisisitiza kuwa mafanikio ya chanjo hayapaswi kupimwa kwa takwimu pekee bali kwa kuhakikisha kila mtoto anafikiwa bila kuachwa nyuma.

“Lengo letu si kufikia asilimia tu, bali kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo stahiki kwa wakati. Hii inawezekana pale viongozi wanapokuwa na uelewa sahihi na kusimamia kikamilifu huduma hizi,” alisema Arope.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo pia yanawalenga kuwajengea viongozi uwezo wa kupanga bajeti, kusimamia rasilimali na kutumia takwimu sahihi katika kubaini maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za chanjo.

Aidha, alionya kuwa uelewa mdogo wa baadhi ya viongozi unaweza kuathiri upangaji wa mipango ya afya na kugawa rasilimali, jambo linaloweza kudhoofisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Katika mtazamo wa washiriki, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Japheth Simeo, alisema mafunzo hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kubaini changamoto halisi na kujifunza mbinu bora za kuzitatua.

“Tunajifunza namna ya kuwabaini watoto ambao hawajapata chanjo na sababu zake, ikiwemo changamoto za usafirishaji, uhifadhi pamoja na mitazamo ya baadhi ya jamii,” alisema Simeo.

Alieleza kuwa viongozi pia wanapatiwa mbinu za kuimarisha mawasiliano na jamii ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa chanjo na kuondoa dhana potofu zinazoweza kuwazuia wananchi kujitokeza kupata huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Simeo, mafunzo hayo yanasisitiza utoaji wa chanjo zote zaidi ya 14 zinazotolewa nchini kwa utaratibu wa kawaida, sambamba na matumizi ya huduma za mkoba kuwafikia wananchi wanaoishi mbali na vituo vya afya.

“Tunajifunza pia kufanya tathmini za mara kwa mara kubaini watoto waliokosa chanjo na kuweka mikakati ya kuwafikia kwa haraka, hatua itakayosaidia kupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa,” aliongeza.

Kwa pamoja, Wizara ya Afya na TAMISEMI zimeeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuimarisha mfumo wa afya nchini, kwa kuweka msisitizo kwenye usimamizi thabiti, matumizi sahihi ya takwimu na upangaji bora wa rasilimali.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuhitimishwa kwa kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuongeza ufanisi wa huduma za chanjo, huku serikali ikitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo zote kwa wakati.

Kwa ujumla, hatua hiyo inaashiria dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania analindwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, bila kujali mazingira anayoishi.






Ends..

Post a Comment

0 Comments