RC MAKALA ACHACHAMAA ,AKERWA VIONGOZI WA MILA KUINGILIA IMANI ZA WAUMINI KANISANI

 RC Makalla Achachamaa, Akemea Vikali Viongozi wa Mila Kuingilia Imani za Waumini Kanisani

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla, ameibuka kwa kauli kali na ya msisitizo akilaani na kukemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa kimila wanaodaiwa kuingilia uhuru wa kuabudu kwa waumini wa dini, ikiwemo kuwajeruhi, kuwakamata viongozi wa dini na hata kufungia makanisa kutokana na masuala ya mila na tohara.

Akizungumza kwa msisitizo mkubwa katika kikao chake na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali mkoani hapa, kilichofanyika Jumanne Machi 31, 2026, Makalla alionyesha wazi kukerwa na mwenendo huo, akieleza kuwa unavunja misingi ya sheria, haki za binadamu na uhuru wa kuabudu unaolindwa kikatiba.

Makalla alisema hatua za baadhi ya viongozi wa kimila kuvamia ibada, kuingilia mafundisho ya kanisa na kuchukua sheria mkononi kwa kufunga makanisa ni vitendo vya kihalifu visivyoweza kuvumiliwa katika jamii inayozingatia utawala wa sheria.

“Hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kuingilia imani ya mwenzake. Hili la kuwakamata viongozi wa dini, kuwajeruhi na kufunga makanisa kwa kisingizio cha mila na tohara halikubaliki kabisa. Hawa ni wahalifu na lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria,” alisisitiza Makalla kwa ukali.

Kwa msisitizo huo, aliagiza Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuchukua hatua za haraka kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote wanaojihusisha na vitendo hivyo, akionya kuwa serikali haitavumilia uvunjifu wa amani kwa kisingizio chochote kile.

Aidha, RC Makalla aliwataka Wakuu wa Wilaya zote mkoani humo kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maagizo hayo, pamoja na kuitisha vikao vya pamoja vinavyowakutanisha viongozi wa dini na wale wa kimila ili kujenga uelewano na kuondoa migogoro inayoibuka.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa amani na mshikamano, huku akiwataka kujiepusha na migogoro ya ndani inayoweza kudhoofisha taasisi zao na kuchochea mpasuko katika jamii.

Makalla alihitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali ya mkoa itaendelea kusimamia kwa karibu hali ya amani na utulivu, akibainisha kuwa Arusha haitakuwa sehemu ya kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyotishia mshikamano wa wananchi na uhuru wa kuabudu.




Kauli hiyo imekuja wakati ambapo kumekuwa na malalamiko ya ongezeko la matukio ya mvutano kati ya baadhi ya makundi ya kimila na taasisi za dini, hali inayohitaji hatua za haraka za serikali kurejesha utulivu na kulinda haki za kila mwananchi.

Ends..

Post a Comment

0 Comments