SARAH ALEX KUPOKEWA KWA KISHINDO ARUSHA BAADA YA KUPOTEZA DAR DERBY

 Sarah Alex Kupokewa kwa Kishindo Arusha Baada ya Dar Derby

By Arushadigital|Dar Ea Salaam

Licha ya kupoteza pambano lake kubwa la Dar Derby lililofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 21 Machi 2026, bondia maarufu kutoka Arusha, Sarah Alex, anatarajiwa kupokewa kwa kishindo kesho katika jiji la Arusha.

Sarah alipanda ulingoni akiwa na matumaini makubwa ya ushindi, lakini alikumbana na upinzani mkali uliomfanya kupoteza pambano hilo lililovuta hisia za mashabiki wengi wa ngumi nchini. Hata hivyo, matokeo hayo hayajapunguza heshima na mapenzi aliyonayo kwa mashabiki wake, hasa wa Arusha ambao wameandaa mapokezi makubwa ya kumtia moyo.

Kwa mujibu wa waandaaji wa mapokezi hayo, msafara mkubwa wa mashabiki, wadau wa michezo pamoja na viongozi wa mkoa unatarajiwa kujitokeza kumpokea bondia huyo kama ishara ya kuthamini juhudi zake na moyo wa kupambana aliouonesha ulingoni.

Akizungumza baada ya pambano hilo, Sarah aliahidi kurejea mazoezini haraka ili kujipanga kwa mapambano yajayo, akisisitiza kuwa kushindwa ni sehemu ya mchezo na kwamba bado ana ndoto ya kufika mbali zaidi katika tasnia ya ngumi.

Mapokezi hayo yanatajwa kuwa sio tu ya kumpongeza kwa ushiriki wake katika pambano kubwa, bali pia ni njia ya kumtia nguvu kisaikolojia ili arejee akiwa imara zaidi na kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye medani za kimataifa.

Post a Comment

0 Comments