SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA MKANDARASI UJENZI WA BARABARA ZA AFCON 2027 ARUSHA

NA JOSEPH NGILISHO | ARUSHA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, ameipa onyo kali kampuni ya China Railway Construction Engineering Group kuhakikisha inakamilisha kwa wakati ujenzi wa miundombinu ya barabara zinazoelekea na kuzunguka uwanja mpya wa michezo unaotarajiwa kutumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 katika Jiji la Arusha.

Akizungumza Machi 20, 2026 jijini humo mara baada ya kushuhudia hafla ya utiaji saini wa mkataba wa uboreshaji wa barabara hizo, Prof. Shemdoe alisema wazi kuwa serikali haitavumilia ucheleweshaji wowote wa mradi huo, akisisitiza kuwa mwisho wa utekelezaji ni Mei 2027 bila kuongeza muda kwa mkandarasi.

“Mkandarasi, barabara hizi tulizosaini mikataba ya ujenzi wake leo zinapaswa kukamilika ifikapo Mei 2027, na hakutakuwa na muda wa nyongeza. Tunahitaji ubora na kasi inayolingana na hadhi ya mashindano haya makubwa ya bara la Afrika,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo si tu maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, bali pia ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza uchumi wa jiji la Arusha pamoja na maeneo jirani.

Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo, akieleza kuwa uwekezaji huo ni uthibitisho wa dhamira ya serikali katika kuendeleza sekta ya michezo na miundombinu nchini.

Aidha, alibainisha kuwa barabara zinazojengwa chini ya usimamizi wa TARURA zina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, ikiwemo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma za kijamii na kuongeza fursa za ajira.

Mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya miundombinu katika Jiji la Arusha, ambalo linajiandaa kuwa moja ya vituo muhimu vya mashindano ya AFCON 2027, huku ukitarajiwa kuongeza mvuto wa uwekezaji, utalii na biashara katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania.

Ends..