SARAH ALEX APATA MAPOKEZI YA KISHINDO ARUSHA, SERIKALI YAJIPANGA KUINUA NGUMI ZA WANAWAKE KUINUA NGUMI ZA WANAWAKE

  SARAH ALEX APATA MAPOKEZI YA KISHINDO ARUSHA, SERIKALI YAJIPANGA KUINUA NGUMI ZA WANAWAKE KUINUA NGUMI ZA WANAWAKE

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 



Jiji la Arusha limeandika ukurasa mpya katika historia ya michezo baada ya bondia wake mahiri, Sarah Alex, kupokewa kwa kishindo kufuatia kurejea kutoka jijini Dar es Salaam alikoshiriki pambano kubwa la kimashindano lililojulikana kama “Dar Derby” mnamo Machi 21, 2026.

Licha ya kupoteza pambano hilo kwa pointi dhidi ya mpinzani wake chini ya promosheni ya kampuni ya Pick Time, Sarah ameendelea kuwa gumzo kutokana na kiwango kikubwa cha ushindani alichoonyesha ulingoni, hali iliyochochea mamia ya mashabiki na wadau wa michezo kujitokeza kumpokea kama shujaa.

Akizungumza mara baada ya kuwasili Arusha, Sarah Alex hakuficha hisia zake za shukrani kwa Watanzania, mashabiki na viongozi wa michezo waliomuunga mkono, akieleza kuwa pambano hilo lilikuwa na ushindani mkubwa na limemjengea uzoefu muhimu katika safari yake ya ngumi.

“Nilipata nafasi ya kupigana pambano kubwa, ushindani ulikuwa mkali sana. Ni kweli sikushinda, lakini najivunia kiwango nilichoonyesha. Hii ni hatua muhimu kwangu kujifunza na kujipanga kwa mapambano yajayo,” amesema Sarah.

Pamoja na hayo, ametoa wito kwa wadau wa michezo nchini kuongeza uwekezaji katika mchezo wa ngumi, hususan kwa wanawake, akieleza kuwa bado wanakumbana na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa vifaa na mazingira rafiki ya mazoezi.

Kwa upande wake, Afisa Michezo na Utamaduni wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, alimpongeza Sarah kwa ujasiri na juhudi alizoonyesha, akisisitiza kuwa kushindwa si mwisho bali ni sehemu ya mafanikio.

“Tunajivunia sana Sarah Alex. Ameonyesha kiwango kikubwa na kutangaza vyema Arusha. Sisi kama jiji tutaendelea kusapoti mashindano ya ngumi ili kuinua kiwango cha mchezo huu na kuibua vipaji vipya,” amesema Maneno.

Ameongeza kuwa serikali ya jiji itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo kuhakikisha mabondia wanapata mazingira bora ya mazoezi pamoja na fursa za kushiriki mashindano ya ndani na nje ya nchi.


Naye Kocha wa bondia huyo, Michael Chika, alieleza masikitiko yake kupoteza pambano hilo lililokuwa la kuwania ubingwa wa Universal Boxing Organization (UBO), lakini akasisitiza kuwa matokeo hayo hayapunguzi uwezo wa bondia wake.

“Kwa kweli tulijiandaa vizuri na tulikuwa na matumaini makubwa ya ushindi, lakini matokeo hayakuwa kama tulivyotarajia. Hata hivyo, Sarah bado ni mdogo na ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi.Tutarudi tukiwa na nguvu zaidi,” amesema Chika kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa pambano hilo limekuwa darasa muhimu kwa timu yao na watajipanga upya kwa ajili ya mashindano yajayo, wakilenga kufanya vizuri zaidi na hatimaye kutwaa ubingwa katika fursa zijazo.

Wakati huo huo, mdau wa michezo na shabiki wa ngumi kutoka Arusha, Rosemary Masawe, amesema matokeo ya kushindwa hayapaswi kukatisha tamaa, bali yawe chachu ya mafanikio ya baadaye.

“Ni kweli tumepoteza, lakini tumerudi na ari mpya. Hii ni sehemu ya kujifunza. Tukipata nafasi nyingine, tutahakikisha tunafanya vizuri zaidi,” amesema Rosemary.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi kubadili mtazamo wao kuhusu wasichana kushiriki ngumi, akisisitiza kuwa mchezo huo unaweza kuwa ajira na chachu ya maendeleo kwa mabinti wengi.

“Ngumi si uhuni kama wengi wanavyodhani. Inaweza kubadilisha maisha ya binti. Tunahitaji kuhamasisha zaidi mashuleni ili kuibua vipaji vipya,” ameongeza.

Kwa ujumla, tukio hilo limeibua upya mjadala wa umuhimu wa kuwekeza katika michezo ya wanawake, hususan ngumi, huku Arusha ikionyesha dhamira ya dhati ya kuwa kitovu cha kukuza vipaji na kuinua hadhi ya mchezo huo nchini.








Ends..

Post a Comment

0 Comments