KIJANA AKAMATWA KWA KUMWINGIZIA UUME MDOMONI ILI APATE UTAJIRI

 KIJANA TABORA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMDHULUMU MTOTO KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

Na ArushaDigital – Tabora


Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia kijana mmoja mwenye umri wa miaka 18, Ibrahimu Kitundu, mkazi wa Kata ya Ipuli, kwa tuhuma za kumfanyia mtoto kitendo cha udhalilishaji wa kijinsia kinachodaiwa kuhusishwa na imani potofu za kishirikina.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, tukio hilo lilitokea Machi 22, 2026 majira ya saa sita mchana katika Mtaa wa Nyerere, Manispaa ya Tabora. Kamanda Abwao alisema kuwa mtuhumiwa anadaiwa kumchukua mtoto huyo kutoka nyumbani kwao na kumpeleka katika kibanda kinachotumika kurushia nyimbo za filamu kilichopo jirani na makazi yao.

Akiwa huko, mtuhumiwa anadaiwa kumdanganya mtoto huyo na kumfanyia kitendo hicho kinyume na maadili. Baadaye alimuacha mtoto huyo katika hali mbaya kiafya.

Kamanda Abwao alieleza kuwa wananchi waliokuwa karibu walipata shaka baada ya kumuona mtuhumiwa akiwa na mtoto huyo, ndipo walipoamua kumfuatilia. Walipofika katika kibanda hicho, walimkuta mtoto akiwa katika hali ya kuugua na kutapika, hali iliyosababisha tukio hilo kuripotiwa mara moja kwa vyombo vya dola.

Katika mahojiano ya awali, mtuhumiwa alikiri kutenda kitendo hicho na kudai kuwa alishawishiwa na mtu mwingine kutoka kwenye kikundi cha sanaa anachoshiriki, kwa madai ya kutimiza masharti ya mganga ili kupata mafanikio katika kazi ya uigizaji. Hata hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi kubaini ukweli wa madai hayo pamoja na kuwabaini wahusika wengine wanaoweza kuhusika.

Kamanda Abwao amesisitiza kuwa chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na imani potofu za kishirikina na kuonya jamii kuachana na vitendo vya aina hiyo vinavyokiuka sheria na haki za binadamu, hususan kwa watoto.

Amesema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa katika kituo cha polisi, huku taratibu za kisheria zikiendelea ili kuhakikisha haki inatendeka.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini viashiria vya vitendo vya ukatili au unyanyasaji, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kulinda usalama wa jamii.

Post a Comment

0 Comments