MBUNGE NGORONGORO AANZISHA MFUKO MAALUM WA ELIMU KUNUSURU NDOTO ZA WANAFUNZI 280
Na Joseph Ngilisho| NGORONGORO,
KATIKA hatua inayolenga kupunguza pengo la elimu na kuinua matumaini ya watoto kutoka familia zenye kipato cha chini, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, ameanzisha mfuko maalum wa elimu utakaowanufaisha wanafunzi 280 kutoka wilayani humo.
Mpango huo unalenga kuwafikia angalau wanafunzi 10 kutoka kila kata, hasa wale wanaotoka katika mazingira magumu ya kiuchumi, ili kuwawezesha kuanza na kuendelea na masomo ya sekondari bila vikwazo vya kifedha.
LAkizungumza kuhusu dhamira hiyo, Ndoinyo alisema mfuko huo umebuniwa kama jibu la changamoto ya muda mrefu inayowakabili wakazi wengi wa Ngorongoro, ambao hutegemea zaidi ufugaji kama chanzo kikuu cha kipato—hali inayosababisha baadhi ya watoto kushindwa kuendelea na elimu ya juu zaidi.
“Tunataka kuhakikisha kila mtoto mwenye uwezo wa kusoma hapotezi ndoto zake kwa sababu ya umasikini. Huu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa jamii yetu,” alisisitiza Ndoinyo.
Katika kuanzisha utekelezaji wake, mbunge huyo ameitisha kikao maalum kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ya elimu, wakiwemo wawekezaji wa sekta ya utalii, taasisi za kifedha na mashirika ya umma. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuweka mikakati madhubuti ya kuanzisha, kuendesha na kuhakikisha uendelevu wa mfuko huo.
Mfuko huo unatarajiwa kugharamia mahitaji muhimu ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari, ikiwemo sare za shule, vifaa vya kujifunzia, ada na gharama nyingine za msingi, ili kuwawezesha kuanza safari yao ya elimu kwa utulivu na ari mpya.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Mohamed Hussein, aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, aliipongeza hatua hiyo huku akibainisha kuwa Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu nchini.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ajira za walimu zaidi ya 20,000, ujenzi wa madarasa zaidi ya 30,000 pamoja na mabweni kwa wanafunzi kutoka jamii za wafugaji—hatua zinazolenga kuongeza upatikanaji na ubora wa elimu nchini.
Katika kuhakikisha mafanikio ya mfuko huo, viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro wameahidi kusimamia utekelezaji wake kwa misingi ya uwazi, uwajibikaji na uadilifu wa hali ya juu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Manja Yaile, alisema wataweka mifumo madhubuti ya usimamizi ili kuhakikisha kila rasilimali inayotolewa inawafikia walengwa waliokusudiwa.
“Tutahakikisha mfuko huu unakuwa wa kuaminika na wenye matokeo chanya yanayoonekana. Kila mdau atakayechangia ataona mabadiliko halisi kwa wanafunzi wanaonufaika,” alisema.
Mbali na kusaidia gharama za elimu, mfuko huo pia unatarajiwa kuwa chachu ya fursa kwa vijana wa Ngorongoro kwa kuwaunganisha na programu mbalimbali za ufadhili wa masomo, ikiwemo Samia Scholarship, pamoja na fursa nyingine za kitaaluma na maendeleo binafsi.
Hatua hii inaonekana kuwa mwanga mpya kwa mamia ya watoto wa Ngorongoro, ambapo sasa wanaweza kuona ndoto zao za elimu zikianza kupata uhalisia, licha ya changamoto za kiuchumi zinazozikabili familia zao.
Ends..




0 Comments