KAMATI YA BUNGE YAIBANA SERIKALI: TAARIFA ZA UWEKEZAJI ZITANGAZWE HOSPITALINI, UPUNGUFU WA WATAALAM WA GANZI WATAJWA
Na Joseph Ngilisho | Dar es Salaam
SERIKALI imepewa maelekezo mazito ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini, ikiwemo kutangaza wazi uwekezaji mkubwa unaofanywa katika hospitali za rufaa ili kuongeza mwitikio wa wananchi kutumia huduma hizo.
Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lukumay, wakati wa ziara ya ukaguzi iliyofanyika Machi 18, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Lukumay alisema licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bado wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu maboresho hayo, jambo linalopunguza matumizi ya huduma zilizoboreshwa.
“Ni muhimu hospitali zetu zikawa na utaratibu wa kutangaza wazi uwekezaji huu—kwa mabango, vipeperushi na njia nyingine—ili wananchi wajue na wajitokeze kupata huduma kwa wakati,” alisema Dkt. Lukumay.
UPUNGUFU WA WATAALAM WABAINISHWA
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imeelekeza Serikali kuongeza idadi ya watumishi wa afya, ikitoa kipaumbele kwa wataalamu wa ganzi na usingizi (anesthesia), ambao ni muhimu katika huduma za upasuaji na matibabu ya dharura.
Alisisitiza kuwa uhaba wa wataalamu hao unaathiri kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma muhimu, hasa katika hospitali za rufaa na zile zinazopokea wagonjwa wengi wa dharura.
DAWA ZA DHARURA NA MIUNDOMBINU
Kamati hiyo pia imeitaka Serikali kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kutosha katika vitengo vya dharura, ikieleza kuwa ucheleweshaji wa dawa unaweza kusababisha kupotea kwa maisha ambayo yangeweza kuokolewa.
Sambamba na hilo, imeagiza hospitali zote nchini kutenga fedha kupitia mapato ya ndani na ruzuku ya Serikali ili kuboresha miundombinu, ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango kabambe (Master Plan) ya ujenzi wa majengo ya kisasa ya ghorofa yatakayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
MWANANYAMALA WAIBUKA KINARA USAFI
Katika ziara hiyo, Dkt. Lukumay aliipongeza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala kwa kiwango cha juu cha usafi na mpangilio wa huduma, akizitaka hospitali nyingine nchini kuiga mfano huo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka motisha kwa watumishi wa afya pamoja na utaratibu wa sare maalum za kazi ili kuimarisha nidhamu, kuongeza ufanisi na kuboresha taswira ya sekta hiyo kwa umma.
SERIKALI YAAHIDI UTEKELEZAJI
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, aliishukuru Kamati hiyo kwa maelekezo yake na kuahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi kwa vitendo.
Alisema maelekezo hayo yanalenga kuimarisha huduma za afya nchini na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi, akiwataka watumishi wa sekta ya afya kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na kwa wakati. Hivyo, kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya taaluma,” alisema Dkt. Samizi.
Kwa ujumla, ziara hiyo imeweka bayana changamoto na mafanikio ya sekta ya afya, huku ikitoa mwelekeo mpya wa maboresho yanayolenga kuongeza upatikanaji, ubora na ufanisi wa huduma za afya nchini.
Ends..


0 Comments