JESHI LA POLISI ARUSHA LATEKELEZA MATENDO YA HURUMA SIKU CHACHE KABLA YA EID EL-FITR

 JESHI LA POLISI ARUSHA LATEKELEZA MATENDO YA HURUMA SIKU CHACHE KABLA YA EID EL-FITR

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanya matendo ya huruma ikiwa ni siku chache kabla ya sikukuu ya Eid El-Fitr, kwa kutembelea vituo vya watoto wenye uhitaji na kutoa msaada wa vitu mbalimbali, hatua iliyogusa mioyo ya wengi na kuonesha mfano bora wa mshikamano wa kijamii.

Katika ziara hiyo ya kibinadamu, askari wa Jeshi hilo walifika katika vituo vya Ummu Aisha na Kindness Children Care, ambapo walikabidhi msaada wa mavazi, vyakula na vifaa vya usafi, wakilenga kushirikiana na watoto hao katika maandalizi ya kusherehekea sikukuu hiyo muhimu ya Kiislamu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zauda Mohamed, amesema hatua hiyo ni sehemu ya wajibu wa Jeshi la Polisi katika kuimarisha uhusiano na jamii pamoja na kuonesha upendo kwa makundi yenye uhitaji.

Amesema sikukuu kama Eid El-Fitr ni kipindi cha furaha kwa Waislamu, hivyo ni muhimu kuhakikisha hata wale walioko katika mazingira magumu wanapata nafasi ya kushiriki furaha hiyo.

“Tumeliona hili kama jukumu letu la kijamii. Tumeamua kushiriki nao kwa vitendo ili kuwapa faraja na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya jamii,” amesema ACP Zauda.

Aidha, ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo taasisi, makampuni na watu binafsi kujenga utamaduni wa kuwajali wahitaji, akisisitiza kuwa mshikamano wa kijamii ni msingi muhimu wa amani na maendeleo.

Kwa upande wao, viongozi wa vituo hivyo wameeleza kufurahishwa na msaada huo, wakisema umeleta matumaini mapya kwa watoto pamoja na kuwapa motisha walezi wanaowahudumia.

Meneja wa Kituo cha Ummu Aisha, Bw. Ally Shemkande amesema msaada huo haujaleta tu mahitaji muhimu bali umeongeza hali ya kuthaminiwa kwa watoto hao, jambo linalochangia ustawi wao wa kihisia na kijamii.

Naye Mkuu wa Kituo cha Kindness Children Care, Bw. Yohana Mwampamba amelipongeza Jeshi la Polisi kwa moyo wa kujitolea, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwafikia makundi mengine yenye uhitaji.

Baadhi ya watoto walionufaika na msaada huo walionesha furaha yao na kulishukuru Jeshi la Polisi, wakisema msaada huo umewaletea tabasamu na kuwapa matumaini mapya, huku wakiomba ziara kama hizo ziendelee mara kwa mara.

Hatua hiyo imeendelea kuimarisha taswira chanya ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, likionekana si tu kama mlinzi wa amani na usalama, bali pia mdau muhimu katika ustawi wa jamii.







Ends

Post a Comment

0 Comments