WAZIRI WA FEDHA AIPA IAA TUZO YA UONGOZI WA KITAIFA KATIKA UJENZI WA UCHUMI WA KIDIJITALI

Ahimiza tafiti zenye majibu ya changamoto za Taifa, apongeza mfumo bunifu wa masomo ana kwa ana na mtandaoni

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

ARUSHA – Waziri wa Fedha ,Balozi Khamis Omar Mussa (Mb), ameipa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) tuzo ya heshima ya uongozi wa kitaifa kwa mchango wake wa kimkakati katika kujenga uchumi wa kidijitali, kuimarisha nidhamu ya fedha za umma na kuandaa rasilimali watu mahiri kwa maendeleo ya Taifa.


Akisoma taarifa ya waziri  wa fedha ,Naibu waziri , Laurent Luswetula aliyekuwa amemwakilisha  katika Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Shahada ya Uzamili ya IAA, yaliyofanyika katika hotel ya Ngurdoto nje Kidogo ya jiji la Arusha,Waziri Mussa alisema chuo hicho ni miongoni mwa taasisi chache nchini zinazotafsiri kwa vitendo dira ya Taifa ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, ujuzi, ubunifu na teknolojia.


“IAA imejidhihirisha kuwa mhimili muhimu wa Taifa katika kuandaa wataalam wenye weledi, uadilifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za uchumi wa kisasa. Hili ni chuo cha mfano katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali,” alisema Waziri Mussa.

Waziri huyo aliipongeza Menejimenti ya IAA kwa kuimarisha mfumo wa mchanganyiko wa masomo ya ana kwa ana na mtandaoni (blended mode) katika ngazi ya Shahada ya Uzamili, akisema mfumo huo umeongeza upatikanaji wa elimu bila kuathiri ubora, huku ukiwawezesha wataalamu wanaofanya kazi kuendelea na masomo yao kwa ufanisi.


Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na IAA katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, mifumo ya kujifunzia kidijitali, usimamizi wa kitaaluma na huduma za wanafunzi, ili kuongeza ushindani wa chuo hicho kitaifa na kimataifa.


Waziri Mussa alisema mchango wa IAA katika uchumi wa Taifa unaonekana wazi kupitia wahitimu wake wanaofanya kazi katika sekta nyeti ikiwemo uhasibu, fedha, kodi, benki, bima, uchumi, biashara, ununuzi na ugavi, masoko, utalii, TEHAMA na usimamizi wa miradi.


Alisisitiza kuwa wataalamu hao ni nguzo ya ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa fedha za umma, uwajibikaji na uwazi, mambo yanayojenga imani ya wananchi na wadau wa maendeleo.


Katika kauli yake yenye msisitizo mkubwa, Waziri wa Fedha aliwahimiza wahitimu wa Shahada ya Uzamili kuhakikisha tafiti zao zinaelekezwa kwenye kutatua changamoto halisi za Taifa, zikiwemo ajira, usimamizi wa fedha za umma, ukuaji wa uchumi jumuishi, ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia.


“Tasnifu zenu zinapaswa kuwa chachu ya sera bora, maamuzi sahihi na maendeleo endelevu. Taifa linahitaji wasomi wanaotumia maarifa yao kama suluhisho, si kama mapambo ya vyeti,” alisisitiza.


Waziri Mussa alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha mazingira wezeshi ya uchumi, nidhamu ya fedha za umma na maendeleo jumuishi, akibainisha kuwa taaluma zinazofundishwa IAA ni msingi wa matumizi bora ya rasilimali za Taifa.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo, Profesa Eliamani Sedoyeka, alisema IAA imehitimisha jumla ya wahitimu 2,250 wa Shahada ya Uzamili, kati yao wanaume 1,369 (asilimia 60.8) na wanawake 881 (asilimia 39.2), wote wakiwa wameandaliwa kitaaluma na kimaadili.


Alisema chuo kimeendelea kuwekeza katika wahadhiri, tafiti, TEHAMA na miundombinu, ikiwa ni pamoja na kupeleka wahadhiri 115 kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD), kupanua kampasi hadi sita na kutumia zaidi ya Sh bilioni 48 kupitia Mradi wa HEET kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mussa aliwataka wahitimu kuwa waadilifu, wabunifu na wenye kujifunza maisha yote, akisisitiza kuwa wasomi ni injini ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii ya Taifa.










Ends..

Post a Comment

0 Comments