HOTELI YA NGURDOTO YATIKISA KWA UBORA SEKTA YA UTALII ARUSHA,YAJIPANGABKWA AFCON UKUMBI MKUBWA WA WATU 8000 WAVUTIA WENGI

HOTELI YA NGURDOTO YAJIPANGA KIKAMILIFU KUPOKEA WAGENI AFCON

Na Joseph Ngilisho, ARUMERU

HOTELI ya Ngurdoto imetangaza utayari wake wa kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali wakati wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ikieleza kuwa imejiimarisha kwa miundombinu ya kisasa ya malazi, kumbi kubwa za mikutano pamoja na huduma za kimataifa za ukarimu.

Akizungumza leo jijini Arusha katika Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika hoteli hiyo na watu zaidi ya 10,000 kuhudhulia,Mkurugenzi wa Hoteli hiyo ya Ngurdoto,  Joan Mrema, amesema hoteli yao ina miundombinu bora na imara inayoiwezesha kuhudumia idadi kubwa ya wageni kwa wakati mmoja bila kuathiri ubora wa huduma.

Bi. Mrema amesema kwa upande wa malazi, hoteli hiyo ina uwezo wa kulaza wageni wapatao 3,400 kwa wakati mmoja, ikiwa na vyumba vilivyopangwa katika makundi mbalimbali kulingana na hadhi na mahitaji ya wageni.

“Katika kundi la juu kabisa tuna Presidential Villas 15, sambamba na Executive Cottages 30. Aidha, tunazo Deluxe Rooms pamoja na aina nyingine za vyumba vinavyokidhi viwango vya juu vya huduma za kitalii,” amesema.

Ameongeza kuwa Hoteli ya Ngurdoto pia ni kituo muhimu cha mikutano na matukio makubwa, ikijivunia kuwa na kumbi tisa (9) za mikutano, ikiwemo ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuchukua hadi watu 8,000 kwa mkupuo mmoja, hatua inayoiweka hoteli hiyo katika nafasi ya kipekee kuhudumia matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa yanayoambatana na AFCON.

“Pia tunao ukumbi unaoweza kuchukua watu 6,000, mwingine watu 300, pamoja na kumbi ndogo zinazoweza kuhudumia hadi watu 10, kulingana na mahitaji ya tukio husika,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Bi. Mrema, Hoteli ya Ngurdoto imejikita kikamilifu katika sekta ya utalii na ukarimu, huku akieleza kuwa hali ya biashara imeendelea kuimarika na mwelekeo unaonyesha matumaini makubwa ya ukuaji, hususan katika kipindi hiki cha maandalizi ya mashindano ya AFCON.

Ameongeza kuwa sekta ya kilimo ni miongoni mwa maeneo yanayonufaika moja kwa moja na uwepo wa hoteli hiyo, kutokana na mahitaji makubwa ya mazao na huduma za ndani, hatua inayochangia kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Hoteli ya Ngurdoto inaendelea kutajwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za kuimarisha hadhi ya Jiji la Arusha kama kitovu cha utalii, mikutano mikubwa na michezo barani Afrika.








Ends..

Post a Comment

0 Comments