WAZIRI MKUU AMALIZA KERO YA MBUNGE HOSPITALI YA OLTRUMENT,MBUNGE LUKUMAY AISHUKURU SERIKALI AOMBA TENA BARABARA ZA LAMI NA SOKO WANANCHI WAMSHANGILIA

 WAZIRI MKUU AMALIZA KERO YA MBUNGE HOSPITALI YA OLTRUMENT,MBUNGE LUKUMAY AISHUKURU SERIKALI KWA UTATUZI WA HARAKA WA KERO ZA WANANCHI

Na Joseph Ngilisho-ARUMERU


MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amemshukuru Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kushughulikia kwa haraka kero ya barabara ya kilometa 1.5 inayoelekea Hospitali ya Wilaya ya Oltrument pamoja na ujenzi wa uzio wa hospitali hiyo, hatua iliyolenga kuimarisha huduma za afya na usalama wa wagonjwa.

Shukrani hizo zilitolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Oltrumenti katika mji mdogo Ngaramtoni wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu mkoani Arusha, ambapo Mbunge Lukumay alisema utekelezaji wa maelekezo hayo umetokana na ziara ya Waziri Mkuu hospitalini hapo na kupokea ombi rasmi la ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami na uzio wa hospitali.


Katika majibu yake, Waziri Mkuu aliuagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kuitisha mkandarasi mara moja ili kuanza matengenezo ya kipande hicho cha barabara, akisisitiza umuhimu wake kwa akina mama wajawazito wanaokwenda kujifungua.

"Meneja Tarura nenda katafute mkandarasi , naibu wa fedha upo hapa tafuteni fedha ili kipande hicho cha Lami kimaliziwe na hili halihitaji mchakato wa maombi ya kibali wizarani ,tayari kibali nimekitoa mimi"Alisisitiza Mwigulu

 Aidha, alielekeza ujenzi wa uzio wa hospitali kufanywa kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri, agizo ambalo Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, aliahidi kulisimamia utekelezaji wake mara moja.


Akizungumza mbele ya wananchi, Dkt. Lukumay pia aliipongeza serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika jimbo hilo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 69.9 katika sekta za afya, maji, elimu ,miundo mbinu na nishati unaonyesha dhamira ya dhati ya serikali kuboresha maisha ya wananchi.

Mbunge huyo alieleza maendeleo ya mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na serikali na kupita katika kata za Kimnyak, Sambasha, Tarakwa, Olirya na Kiranyi, wenye thamani ya shilingi bilioni 520, ambapo shilingi bilioni 2.7 tayari zimeidhinishwa kwa ajili ya ununuzi wa mabomba ili kusambaza maji katika kata hizo zinazopitiwa na mradi huo.

Alisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya maji yenye kiwango kikubwa cha flouride, hususan katika kata za Oldonyosambu  na Oldonyowasi.

Katika sekta ya miundombinu ya barabara, Dkt. Lukumay alibainisha umuhimu wa barabara mbalimbali zikiwemo Mwandeti–Kilimamoto Loning'o–Seliani na Sambasha–Olmotonyi–Ngaramtoni ,Barabara ya Sekei-Olgilai , akieleza kuwa miradi hiyo itarahisisha usafiri wa wananchi na kuchochea utalii katika eneo hilo lenye vivutio vya asili.

“Miradi hii ni uti wa mgongo wa maendeleo ya wananchi wetu. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usikivu na hatua za haraka zinazotoa matumaini mapya kwa jamii,” alisema Mbunge Lukumay.

Pia aliomba soko la Ngaramtoni liweze kuboreshwa kwa kiwango cha juu ili kuvutia watalii mbalimbali wanaofika katika jimbo hilo hatua ambayo waziri Mkuu aliagiza majiji na manispaa kuainisha maeneo ya masoko na kuyafanyia maboresho ya kina.

....Ends.....

Awali Mgamga Mfawidhi WA hospital ya Oltrument,Dkt Lootosim Zabroni alisema changamoto kubwa katika hospitali hiyo ni ukamllishaji wa kipande hicho cha barabara kwa kiwango cha Lami pamoja na ujenzi wa uzio unaokisiwa kugharimu kiasi cha sh,milioni 316,000.

Pia Dkt Zabroni hakusita kuishukuru serikali kwa kupeleka fedha  kiasi cha sh,bilioni 1.465 kwa ajili ya kuboresha huduma na miundombinu ya hospitali.

Ziara ya Waziri Mkuu Arumeru Magharibi imewapa wananchi fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa serikali huku wakishuhudia utekelezaji wa maamuzi ya haraka yanayolenga kuboresha huduma za msingi katika sekta za afya, maji na miundombinu.




..Ends..

Post a Comment

0 Comments