Na Joseph Ngilisho – ARUMERU
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasary, amewasilisha kilio cha wananchi wa jimbo lake akiiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya barabara, maji na huduma za jamii ili kuendana na kasi ya maendeleo inayoshuhudiwa katika mkoa wa Arusha.
Nasary alitoa ombi hilo mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa wa elimu na utafiti unahitaji kuungwa mkono na miundombinu imara itakayowanufaisha wananchi na taasisi zilizopo Arumeru.
Alisema wananchi wanahitaji kukamilishwa kwa barabara zinazounganisha maeneo ya Tengeru, Mbuguni na Mirerani pamoja na barabara mbadala zinazopunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, watalii na huduma za kijamii.
“Maendeleo ya elimu ya juu na uwekezaji wa kitaifa yanahitaji kuungwa mkono na miundombinu ya uhakika ili wananchi wanufaike kikamilifu na fursa zilizopo,” alisema Nasary.
Mbunge huyo alieleza kuwa uwepo wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela umeifanya Arumeru kuwa kitovu cha elimu ya sayansi na teknolojia barani Afrika, huku ikivutia wanafunzi na watafiti kutoka mataifa mbalimbali.
Alisema hadhi hiyo inaleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo, hivyo ni muhimu kuimarisha barabara, huduma za maji na miundombinu mingine inayozunguka taasisi hiyo.
Nasary alisisitiza umuhimu wa kuharakishwa kwa miradi ya maji katika baadhi ya vijiji vya Arumeru Mashariki, akieleza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama bado ni changamoto kwa wananchi wengi.
Aidha, aliomba Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya na kuimarisha upatikanaji wa huduma za dharura, akisema hatua hizo zitasaidia kulinda ustawi wa jamii na kuongeza tija ya wananchi kiuchumi.
Pamoja na kuwasilisha mahitaji ya wananchi, Mbunge huyo aliipongeza Serikali kwa uwekezaji unaoendelea katika elimu ya juu, miundombinu na huduma za jamii, akisema matokeo ya miradi hiyo yanaanza kuonekana katika maisha ya wananchi wa Arumeru na mkoa wa Arusha kwa ujumla.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, alisema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 3.81, ambapo tayari ujenzi wa mita 500 umeanza.
Aliongeza kuwa mapema mwezi Machi ujenzi wa mita 700 ambazo usanifu wake umekamilika utaanza akisisitiza kuwa tayari fedha zimetengwa na mkandarasi yupo eneo la kazi akiendelea na utekelezaji katika kipande chenye urefu wa kilometa 1.2.
Ziara ya Waziri Mkuu katika taasisi hiyo imelenga kukagua maendeleo ya elimu ya juu na kuhimiza ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za utafiti katika kuendeleza uchumi unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia.
Ends .

0 Comments