WAANDISHI WA HABARI WANUSURIKA KIFO KWA AJALI WAKITOKA MAADHIMISHO YA MIAKA 49 YA CCM

WANAHABARI IRINGA WAPATA AJALI BAADA YA MAADHIMISHO YA MIAKA 49 YA CCM

Na Arusha Digital – Iringa

BAADHI ya waandishi wa habari pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa wamepata ajali ya gari leo Februari 5, 2026, walipokuwa wakirejea kutoka kwenye sherehe za Maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho, yaliyofanyika kimkoa katika Kata ya Idodi, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Taarifa zilizothibitishwa zinaeleza kuwa ajali hiyo ilihusisha gari lililokuwa likiwabeba viongozi na waandishi wa habari waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kikazi wakati wa maadhimisho hayo. Ndani ya gari hilo alikuwapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Joseph Nzala Lyata, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa na mwandishi wa magazeti ya Serikali, Frank Leonard.

Waandishi wengine waliokuwemo kwenye gari hilo ni Denis Mlowe wa Fullshangwe Blog, Clement Sanga wa Channel Ten, Herieth Mola wa Mkombozi Online TV, Zuhura Zukheri wa Abood TV, pamoja na wadau wengine wa tasnia ya habari.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, hakuna kifo chochote kilichoripotiwa kufuatia ajali hiyo. Hata hivyo, mamlaka husika zinaendelea kukusanya taarifa ili kubaini idadi kamili ya majeruhi na hali zao kiafya.

Vyombo vya usalama vimeanza uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo, huku jitihada za kutoa msaada na kufuatilia hali za waathirika zikiendelea.

Tutazidi kuwafahamisha wasomaji wetu pindi taarifa zaidi zitakapopatikana.

Post a Comment

0 Comments