MAKAMPUNI 408 YA TANZANIA YAFUNGULIWA MLANGO SOKO LA MAZAO CHINA,TPHPA YABAINISHA MAZAO 12 YALIYORUHUSIWA SOKO LA CHINA

MAKAMPUNI 408 YA TANZANIA YAFUNGULIWA MLANGO SOKO LA CHINA

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

SERIKALI ya Tanzania imefanikiwa kufungua rasmi soko kubwa la China kwa makampuni ya ndani 408 ya mazao ya kilimo, hatua inayotajwa kuwa mapinduzi makubwa katika biashara ya kimataifa na diplomasia ya kiuchumi ya Taifa.

Hatua hiyo imetokana na ushirikiano wa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ubalozi wa Tanzania nchini China pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, ambapo makampuni hayo yamesajiliwa katika mfumo wa Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GACC).

Akizungumza na waandishi wa habari leo februali 5,2026  katika ofisi kuu za Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) mkoani Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Profesa Joseph Ndunguru, alisema usajili huo umezipa kampuni hizo ruhusa ya kusafirisha mazao ya kilimo moja kwa moja kwenda China.


“Hii ni hatua kubwa kwa wakulima, wafanyabiashara na Taifa kwa ujumla. Soko la China ni pana na lenye ushindani mkubwa, hivyo kufunguliwa kwake kunatoa fursa adimu ya kukuza mauzo ya nje na kuongeza pato la Taifa,” alisema Profesa Ndunguru.


Alifafanua kuwa orodha kamili ya makampuni yaliyosajiliwa inapatikana kwenye tovuti rasmi ya TPHPA, akiwahimiza wadau wa kilimo na biashara kuitembelea kwa taarifa zaidi.


Profesa Ndunguru alieleza kuwa usajili huo ni utekelezaji wa masharti ya kimataifa ya Sanitary and Phytosanitary Measures (SPS) pamoja na makubaliano ya kibiashara kati ya Tanzania na China, yanayolenga kuhakikisha mazao yote yanayosafirishwa yanazingatia viwango vya afya ya mimea, ubora na usalama wa chakula kwa mujibu wa soko la China.


Aliwataka wafanyabiashara waliopata fursa hiyo kuendelea kuzingatia masharti yote ya afya ya mimea, mfumo wa ufuatiliaji wa mazao (traceability), matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na taratibu za ukaguzi kabla ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi.








Kwa mujibu wa TPHPA, jumla ya mazao 12 ya kilimo yameruhusiwa kuingia katika soko la China ambayo ni Kakao, Kahawa, Ufuta, Soya, Parachichi, Karanga, Muhogo, Karafuu, Korosho, Mashudu ya Pamba, Mashudu ya Alizeti na Pilipili.


Aidha, Profesa Ndunguru alisema bado kuna fursa kwa makampuni mengine yanayopenda kuingia katika soko la China kuwasilisha maombi yao kupitia TPHPA kwa ajili ya kupata mwongozo wa taratibu za usajili katika mfumo wa GACC.


“Tunawahimiza wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa hii kwa kuongeza uzalishaji, kuzingatia ubora na kushiriki kikamilifu katika minyororo ya thamani,” alisisitiza.


Aliongeza kuwa TPHPA itaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha masharti ya kitaifa na yale ya nchi lengwa yanazingatiwa kikamilifu.


Katika hatua nyingine, Prof. Ndunguru aliishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake ya kufungua na kupanua masoko ya mazao ya kilimo, akisisitiza kuwa TPHPA itaendelea kutafuta masoko mapya duniani kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kukuza mauzo ya nje ya nchi.


Kwa mujibu wa TPHPA, mafanikio hayo yametokana na ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini China, na makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili.


Mchakato wa utekelezaji wa makubaliano hayo ulianza Februari, 2022 na hadi sasa umezaa matunda kwa kufungua fursa kwa makampuni 408 ya Kitanzania kuingia moja kwa moja katika soko la China.


China ikiwa na idadi kubwa ya watu na soko pana, inatajwa kuwa fursa muhimu ya kibiashara itakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo, kuongeza ajira, kukuza kipato cha wakulima na kuimarisha uchumi wa Taifa.


Ends...


Post a Comment

0 Comments