TAZAMA PICHA STENDI MPYA YA MABASI ARUSHA ILIPOFIKIA MAKONDA ATEMBELEA ATAKA IWE FURSA KUBWA ZA KIUCHUMI KWA WANANCHI

 MAKONDA ATAKA  STENDI MPYA YA BASI ARUSHA IWE FURSA KUBWA YA KIUCHUMI KWA WANANCHI

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

ARUSHA: Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema ujenzi wa Stendi Mpya ya Mabasi ya Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayobadilisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa wananchi wa Jiji la Arusha kwa kufungua fursa mpya za ajira, biashara na uwekezaji.


Akizungumza leo Feb. 3,2026 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Stendi Mpya ya Mabasi na Soko la kisasa la Kilombero, Makonda alisema mradi huo ni jibu la kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Arusha waliokuwa wakisubiri kwa miaka mingi kupatikana kwa stendi ya kisasa itakayokidhi mahitaji ya sasa ya usafiri na biashara.


“Kwa miaka mingi wananchi wa Arusha walikuwa wanauliza stendi itajengwa lini. Leo hatuulizi tena, stendi inajengwa sasa. Huu ni ushahidi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali ya vitendo na utekelezaji,” alisema Makonda.

Makonda alisema stendi hiyo mpya haitakuwa tu eneo la kupandia na kushushia abiria, bali itakuwa kitovu kikubwa cha shughuli za kiuchumi, kitakachochochea uanzishwaji wa biashara ndogo na kubwa ikiwemo migahawa, maduka, hoteli, apartments, huduma za usafiri na sekta nyingine zinazohusiana na mzunguko wa watu na fedha.


Alisema ujenzi wa stendi hiyo pamoja na soko la kisasa ni sehemu ya mpango mpana wa kuifanya Arusha kuwa jiji la kibiashara na utalii, linalokwenda sambamba na hadhi yake kama lango la utalii wa kimataifa.


“Miradi hii ni fursa. Serikali haitamchukua mwananchi mkono kumuingizia kipato, bali inatengeneza mazingira na fursa. Sasa ni jukumu la wananchi wa Arusha kuzitumia fursa hizi kufanya kazi, kuwekeza na kuboresha maisha yao,” alisisitiza.


Makonda pia amewahimiza wananchi na wafanyabiashara kuanza kujiandaa mapema kwa kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo yanayozunguka stendi hiyo, akibainisha kuwa thamani ya maeneo hayo itaongezeka mara dufu baada ya mradi kukamilika.


Katika hatua nyingine, Mbunge huyo alipongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha, Jiji la Arusha pamoja na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa kasi na ubora wa kazi, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha mkandarasi analipwa kwa wakati ili mradi ukamilike kwa mujibu wa mkataba.


“Tunataka mkandarasi aendelee kufanya kazi kwa kasi. Serikali iko tayari kutimiza wajibu wake, lakini tunataka mradi huu ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili,” alisema.


Ziara hiyo ni sehemu ya ratiba ya Waziri huyo kukagua na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Jimbo la Arusha Mjini, ikiwa ni pamoja na miradi ya miundombinu, masoko, vituo vya afya na huduma nyingine za kijamii.


Ujenzi wa Stendi Mpya ya Mabasi na Soko la kisasa unatajwa kuwa miongoni mwa miradi itakayochochea kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa Jiji la Arusha, kuongeza mapato ya wananchi na kuiweka Arusha katika ramani ya miji ya kisasa yenye miundombinu rafiki kwa biashara na uwekezaji.



Ends .


Post a Comment

0 Comments