MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA YAIMARIKA: SERIKALI YAANZISHA MADAWATI 115 NCHINI
Na Joseph Ngilisho – Arusha
SERIKALI imeongeza kasi ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuanzisha madawati 115 ya kupinga ukatili katika masoko yaliyopo kwenye mikoa 12 na halmashauri 88 nchini—hatua inayolenga kusogeza huduma za msaada karibu na wananchi na kuwezesha waathirika kupata ulinzi na ushauri kwa haraka zaidi katika maeneo wanayofanya shughuli zao za kila siku.
Akizungumza february 20,2026 jijini Arusha wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC), Dkt. Theresia Kuiwite, Mratibu wa Masuala ya Usalama wa Mazingira na Stadi za Maisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha kinga, ufuatiliaji na utoaji wa huduma rafiki kwa waathirika.
Alisema uwepo wa madawati hayo katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya wananchi umeongeza ujasiri wa waathirika kuripoti matukio na kusaidia mamlaka kuchukua hatua kwa wakati. “Lengo letu ni kujenga mazingira salama kwa wanawake na watoto kwa kuhakikisha msaada unapatikana pale wanapouhitaji zaidi,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Dkt. Kuiwite, Serikali pia imeendesha kampeni pana za uelimishaji zinazojumuisha uwekaji wa mabango 8,015 katika maeneo ya serikali za mitaa, pamoja na midahalo 4,748 iliyolenga kuchambua visababishi vya ukatili na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu njia za kuuzuia.
Aidha, mikutano ya kijamii 61,387 imefanyika katika ngazi za vijiji na mitaa, hatua iliyochochea baadhi ya maeneo kuanza kutunga sheria ndogo za kupinga ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, alibainisha kuwa kasi ya utungaji na utekelezaji wa sheria hizo bado inahitaji kuongezwa ili kufikia vijiji vyote nchini.
Katika kupanua wigo wa huduma za ulinzi, Serikali pia imeanzisha madawati ya Ustawi wa Jamii katika vituo vya mabasi, yakilenga kusaidia waathirika wa ukatili, kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu na kutoa mwongozo kwa makundi hatarishi katika maeneo ya usafiri wa umma.
Kwa upande wa wadau wa maendeleo, UN Women Tanzania imeeleza kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mifumo ya kinga na ulinzi. Akizungumza katika kikao hicho, Lucy Tesha, Ofisa Miradi wa taasisi hiyo, alisema ushirikiano huo unalenga kukuza usawa wa kijinsia na kujenga jamii inayolinda utu na haki za wanawake na watoto.
“Takwimu zinaonesha ukatili wa kijinsia bado ni changamoto ya kimataifa na ya kitaifa. Ndiyo maana tunaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha sera, sheria na huduma za ulinzi kwa makundi hatarishi,” alisema Tesha.
Hatua hizi, kwa pamoja, zinaashiria dhamira thabiti ya Serikali na wadau wa maendeleo ya kijamii katika kujenga jamii salama, yenye heshima kwa utu wa binadamu na inayoweka ulinzi wa wanawake na watoto kuwa kipaumbele cha maendeleo endelevu ya taifa.
Ends .







0 Comments