Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC, Baraka Simon, amesema halmashauri imependekeza bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 75.4 kwa mwaka wa fedha ujao 2026/27 , ikilenga kuimarisha miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza katika Baraza la Bajeti la Madiwani wa Halmashauri hiyo na kusitisha kuwa mgawanyo wa bajeti unahusisha matumizi ya maendeleo, ruzuku za mishahara ya watumishi pamoja na matumizi ya kawaida ya uendeshaji wa halmashauri.
Alisema kati ya bajeti hiyo, mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 927 huku takribani shilingi bilioni 11 zikielekezwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo, hatua inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi na kuendana na mwelekeo wa serikali unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha huduma za kijamii.
Katika sekta ya elimu, halmashauri imeweka kipaumbele katika maandalizi ya ongezeko kubwa la wanafunzi ifikapo mwaka 2027. Arusha DC inatarajia kupokea wanafunzi wapatao 22,000, hali inayoongeza mahitaji ya vyumba vya madarasa zaidi ya 200, maabara, nyumba za walimu pamoja na samani za shule.
Aidha, katika sekta ya afya, halmashauri imepanga kukamilisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, pamoja na kununua vifaa tiba ili kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, taasisi za miundombinu zikiwemo TARURA, AUWSA na REA zimetenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kuboresha barabara, maji na nishati katika kata na vijiji mbalimbali.
Halmashauri pia inapanga kuanzisha vituo vitatu vipya vya ukusanyaji mapato katika maeneo ya Angaramtoni, Kiseria na Kisongo ili kuongeza ufanisi wa mapato na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utagusa sekta zote muhimu za maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Arusha DC.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay,
Alisisitiza umuhimu wa mawasiliano ya karibu kati ya viongozi wa halmashauri hiyo na madiwani ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akionesha masikitiko yake kwa baadhi ya madiwani kutopokea simu anapohitaji taarifa kuhusu hali ya maendeleo na changamoto zilizopo.
Ends..



0 Comments