MEYA ARUSHA ADUWAZWA KATA YA MOSHONO KUNUKA UCHAFU,ATOA SIKU TATU MAWAKALA WA USAFI KUINGIA KAZINI ,AANZISHA MSAKO WA WACHAFUZI WA MAZINGIRA

 MEYA ADUWAZWA NA UCHAFU MOSHONO,ATOA SIKU TATU MAWAKALA WA USAFI KUINGIA KAZINI 


— Aanzisha msako dhidi ya wachafua mazingira, daladala zapigwa faini, wafanyabiashara waamriwa kuwa na vibebea taka

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA

Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha,  Maxmillian Iranqhe, ametangaza msimamo mkali dhidi ya uchafu kwa kuwaagiza mawakala wote wa usafi katika Kata ya Moshono kuanza kazi ndani ya siku nne kuanzia leo.

Alisisitiza kuwa hatavumilia uzembe unaohatarisha afya za wananchi na taswira ya Jiji la Arusha.

Meya Iranqhe alitoa agizo hilo leo Februari 7, 2026, akiwa mgeni rasmi katika Kampeni ya “Ng’arisha Jiji” iliyofanyika Moshono—kampeni inayolenga kusafisha na kulinda mazingira ya Jiji la Arusha, lango kuu la utalii nchini Tanzania.
Akizungumza mbele ya wananchi, viongozi wa kata na wadau wa mazingira, Meya alisema kuwa licha ya kutoa maelekezo hayo wiki iliyopita, utekelezaji wake bado haujaridhisha. 

Hali hiyo, alisema, inaashiria uzembe wa baadhi ya viongozi wa ngazi ya kata katika kuratibu upatikanaji na uanzishaji wa mawakala wa usafi.

“Hakuna sababu ya kuendelea kuchelewa. Ndani ya siku nne kuanzia leo, mawakala wa usafi lazima wawe kazini. Afya ya wananchi na heshima ya jiji letu haviwezi kusubiri,” alisisitiza Meya.

Katika hatua nyingine, Meya Iranqhe aliagiza Idara ya Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Mazingira kuanza kupiga faini daladala ambazo abiria wake wanatupa taka nje ya magari na kuchafua mazingira.

 Alieleza kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, ambaye naye ameagiza Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuanza kukamata magari ya abiria yanayokiuka taratibu za utunzaji wa mazingira.

Hatua hiyo inalenga kukomesha tabia ya kutupa taka hovyo barabarani, hasa kwenye maeneo yenye shughuli nyingi za usafiri, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa uchafu wa jiji.

Meya pia aliwakumbusha viongozi wa Idara ya Afya kuanzia ngazi ya kata hadi mitaa kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Aliwaagiza watoke maofisini na kuwafuata wananchi walipo ili kusimamia kikamilifu usafi wa mazingira na kutoa elimu ya vitendo kuhusu utunzaji wa mazingira.

“Usimamizi hauwezi kufanyika ukiwa ofisini. Lazima muwe mtaani, sokoni na kwenye vituo vya mabasi,” alisema.

Aidha, Meya Iranqhe aliagiza wafanyabiashara wote wasio na vibebea taka (dustbins) katika maeneo yao ya biashara kupigwa faini, akisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja—si serikali pekee.


Akihitimisha, Meya alisisitiza kuwa Jiji la Arusha, kama lango la utalii wa Tanzania, halina budi kuwa safi wakati wote ili kulinda afya za wananchi, kuvutia wageni na kuimarisha taswira ya taifa.

Kampeni ya “Ng’arisha Jiji” inaendelea katika kata mbalimbali jijini Arusha, huku uongozi wa jiji ukiahidi kuchukua hatua kali kwa wote watakaokiuka sheria na taratibu za usafi wa mazingira.

Ends...

Post a Comment

0 Comments