DC MKUDE AWAKOSHA WAFANYABIASHARA ATUMIA DAKIKA 30 KUTATUA MGOGORO SOKO LA KILOMBERO ,AAMURU MAGETI YALIYOFUNGWA KUFUNGULIWA , ASHANGILIWA

DC MKUDE ATUMIA DAKIKA 30 KUTATUA MGOGORO WA WAFANYABIASHARA SOKO LA KILOMBERO ,AAMURU MAGETI YALIYOFUNGWA KUFUNGULIWA , WACHUUZI WOTE KUINGIA NDANI 

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ameuvunja kwa haraka mgogoro uliokuwa ukifukuta kwa muda mrefu kati ya wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda katika Soko namba 68 la Kilombero, kwa kuamuru wachuuzi wote waliokuwa wakipanga bidhaa nje ya soko kuingia mara moja ndani ya soko hilo.


Hatua hiyo ya DC Mkude imekuja baada ya mgogoro huo kuibuliwa hadharani hivi karibuni na mfanyabiashara Salome Mollel, wakati wa mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alipotembelea ujenzi wa soko la kisasa la Kilombero unaoendelea.


Katika maelezo yake, Salome aliiomba Serikali kuwaruhusu baadhi ya wafanyabiashara kupanga bidhaa kando ya barabara, akidai kuwa ndani ya soko kulikuwa kumejaa. 


Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa vikali na wafanyabiashara wenye meza ndani ya soko hilo, waliodai wao hulipa kodi halali na kwamba kuruhusu biashara kufanyika nje ya utaratibu kungewanyima wateja, kushusha mapato yao na hatimaye kuikosesha Halmashauri ya Jiji la Arusha mapato.


Akizungumza leo Februali 7,2026 wakati wa ziara yake ya kutatua kero hiyo, DC Mkude, akiongozana na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya, alitoa maelekezo mazito yaliyoleta shangwe kwa wafanyabiashara, hususan kina mama waliokuwa wamefurika sokoni hapo.


“Wale wote waliopo nje watoke barabarani mara moja waingie ndani ya soko. Namuelekeza Mkurugenzi afungue mageti ili wafanyabiashara waingie ndani, na mkandarasi arudishe nyuma uzio wake wa mabati,” alisema DC Mkude kwa msisitizo huku akishangiliwa kwa shangwe


DC Mkude alipiga marufuku vikali tabia ya kupanga bidhaa chini au katika maeneo yasiyoruhusiwa, akisema hatua hiyo siyo tu inakiuka utaratibu bali pia inahatarisha afya za walaji na usalama wa jiji.


Katika hatua ya mpito, aliamuru mageti ya eneo la mradi wa soko la kisasa kufunguliwa, ili wajasiriamali wasiokuwa na maeneo maalumu waweze kuyatumia kwa muda wakati wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo.


Kwa upande mwingine, DC Mkude aliahidi kuwa wafanyabiashara wote waliopo ndani ya Soko namba 68 watapatiwa mikataba halali ya biashara, huku akionya kuwa wale waliokuwa wamepangisha vizimba au meza zao kwa wengine, umiliki utarejeshwa kwa waliopangishwa ili kurejesha haki na nidhamu ya biashara.


Akigusia changamoto ya umeme sokoni hapo, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wafanyabiashara kuomba mita binafsi za TANESCO, ili kila mfanyabiashara anayehitaji huduma hiyo apatiwe umeme wa uhakika muda wote, tofauti na mfumo wa sasa wa kuwashwa kwa muda maalumu.


Awali, Diwani wa Kata ya Levoloai, Abbas Haji, alimshukuru DC Mkude kwa uamuzi wa kufungua mageti ya soko, akisema hatua hiyo itaondoa msongamano na migogoro isiyo ya lazima.


 Aliwataka wafanyabiashara kuacha kulalamika pembeni na badala yake kufikisha kero zao katika ofisi yake au ofisi ya Mtendaji wa Kata kwa ajili ya kutatuliwa kwa haraka.



Hatua za DC Mkude zimeonekana kurejesha matumaini, utulivu na haki miongoni mwa wafanyabiashara wa Soko la Kilombero, huku zikitafsiriwa kama pigo kwa biashara holela na ushindi kwa utaratibu, afya na mapato ya jiji.






Ends..

Post a Comment

0 Comments